May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli ashauri jeshi kukamata mawaziri

Spread the love

 

JESHI la Magereza nchini Tanzania, limeshauriwa kukamata mawaziri ama makatibu wakuu kwenye taasisi zilizoshindwa kulipa maeni yao. Anaripoti Regina Mkonde, …(endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi tarehe 4 Februari 2021, na Rais wa Tanzania, John Magufuli wakati akizindua Makao Makuu mapya ya jeshi hilo yaliyopo Msalato, Dodoma.

Amesema, viongozi hao wakichukuliwa hatua hiyo, watajifunza kulipa mapema madeni ya taasisi zao.

“Lakini na ninyi si maaskari (Jeshi la Magereza)? ukimshika hata waziri wa taasisi au katibu mkuu unayemdai, ukamuweka mahabusu yenu huko si atatoka kule amelipa?” amehoji Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesisitiza “unajua saa nyingine ni unyama unyama, mnalalamika mno mambo mengine mnayaweza mwenyewe.”

Amesema, kama waziri au katibu mkuu atakamatwa kutokana na suala hilo, kisha akahitaji msaada wake, atanyamaza kimya ili wajifunze kulipa madeni yao.

“Unamshika kule, watapiga kelele mimi nanyamaza. Nitamwambia pole mheshimiwia hawa wanakudhalilisha lakini amekipata cha moto. Sababu saa nyingine watu hawajali.”

“Pesa zinazopatikana kwenye safari, marupurupu yao wanatumia lakini kulipa deni hawalipi. Sababu dawa ya deni ni kulipa, saa nyingine vifujo fojo kidogo vifanyeni,” amesema Rais Magufuli.

Hata hivyo, Rais Magufuli amewaambia kwamba hakuwatuma, na kwamb a kwa njia hiyo wanaweza kulipa.

“Lakini msiseme nimewaambia, ila watawalipa nani anapenda kudhalilika? akaambiwa unahitajika Jeshi la magereza, sababu gani mtajua huko huko,” amesema.

Wakati huo huo, Rais Magufuli ameagiza taasisi zinazodaiwa na jeshi hilo kiasi cha Sh. 10.16, kulipa fedha hizo ndani ya siku 30.

“Tujipe mwezi mmoja hili nitalisimamia mwenyewe ili taaissi zote mnazodai zilipe. Natoa wito kwa taasisi zote zinazodaiwa na magereza ndani ya siku 30, maana yake mwezi mmoja waanze kulipa. La sivyo nitazikata moja kwa moja kupitia hazina na nitazipeleka magereza,” ameagiza Rais Magufuli.

Agizo hilo la Rais Magufuli limetolewa baada ya Waziri wa Mambo ya Nchi, George Simbachawene na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Suleiman Mzee kumuomba atatue changamoto zinalikabili jeshi hilo.

Awali, Simbachawene amemuomba Rais Magufuli kutatua changamoto ya uhaba wa sare za maaskari wa Jeshi la Magereza, kwa kuongeza fedha katika bajeti.

“Jeshi la Magereza wanahitaji Sh.8 bilioni kwa ajili ya uniform za maskari wake, lakini zinazotolewa kwa mwaka ni Sh.163 milioni kutoka Sh.8 bilioni Kwa hiyo upungufu ni mkubwa.”

Pia, Kamanda Mzee amemuomba Rais Magufuli kulifanyia kazi suala la malipo ya wastaafu wa jeshi hilo, pamoja na upungufu wa watumishi.

“Nizungumzie malipo kwa wastaafu, wengine hawajalipwa stahiki zao hii inaleta malalamiko mengi. Wastaafu wa miaka ya nyuma fedha zao zimeingizwa kwenye madeni zinatakiwa kulipwa na hazina.

“Kwa upande wetu sisi tumeendelea kuwalipa wastafau kwa mwaka huu, wote wanaostaafu kuanzia mwezi wa tano tumekuwa tukiwalipa kwa pesa zetu sasa hii inaleta malalamiko kwa wastaafu miaka ya nyuma,” amesema Kamanda Mzee.

Akijibu kuhusu maombi ya kuajiri watumishi wapya, Rais Magufuli alishauri jeshi hilo kuwatumia wafungwa katika shughuli zake za uzalishaji.

“Wafungwa wanaendelea kuongezeka mbali ya wafungwa wengine, tunaweza kuondoa upungufu huo kwa kutumia wafungwa wanaoingia mle, kwani kila mfungwa ana profesion yake,” amesema Rais Magufuli.

Kuhusu changamoto ya malipo kwa wastaafu, Rais Magufuli amemuagiza Simbachawene kufuatilia Wizara ya Fedha na Mipango ili fedha hizo zipatikane.

“Lakini mliniambia juu ya wastaafu 331 wanaodai Sh. 546.1 Mil kwa ajili ya nauli na mizigo yao, hawa wastaafu waziri fuatilia wizara ya fedha ili wastaafu hawa walipwe malipo yao mapema,” ameagiza Rais Magufuli.

Vilevile, Rais Magufuli ameagiza Jeshi la Magereza kuwatumia wafungwa katika kutatua changamoto ya upungufu wa sare za askari wake au waombe msaada kutoka katika majeshi mengine hasa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

“Uniform (sare) mkiamua mtaweza, kweli katika magereza yote hakuna wafungwa wanaojua cherehani kushona? Wote hawa wafungwa hayupo anayejua kukanyaga nguo, ina maana katika nchi hii mafundi cherehani hawafungwi?

“Kama wapo wanaofungwa na kiwanda vipo mnavyojenga, ni kiasi cha kuleta vyerehani tu hata 100 mkanunua majora ya rangi mnayotaka ninyi wafungwa wakaanza kushona,” ameshauri Rais Magufuli.

error: Content is protected !!