RAIS wa Tanzania, John Pombe Magufuli amesema, aligoma kukubali wito wa kukutana na aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad (77), mara baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2015. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Mkuu huyo wa nchi, ametoa siri hiyo wakati anazungumzia kifo cha Maalim Seif, kilichotokea Jumatano ya tarehe 17 Februari 2021, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam, kisha mwili wake kuzikwa Alhamisi ya tarehe 18 Februari mwaka huu, kijijini kwao Nyali Mtambwe, visiwani Pemba.
Akizungumza katika ibada ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, leo Ijumaa tarehe 19 Februari 2021, Rais Magufuli amesema, Maalim Seif alimuandikia barua zaidi ya mara tatu, akimuomba kuonana nae, lakini alisita kukubali.
Ibada ya kuuaga mwili wa Balozi Kijazi, aliyefariki dunia katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma tarehe 17 Februari 2021, ilifanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli amesema, alisita kuonana na Hayati Maalim Seif, aliyekuwa Mgombea Urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, kupitia Chama cha Wananchi (CUF), kufuatia hatua yake ya kugoma kushiriki kwenye uchaguzi wa marudio.
Uchaguzi wa marudio Zanzibar ulifanyika tarehe 20 Machi 2016, baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi huo, uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015.
Jecha alifuta matokeo ya uchaguzi huo, kwa maelezo mchakato wake ulikuwa na dosari nyingi. Lakini Hayati Maalim Seif na CUF waligoma kushiriki uchaguzi wa marudio, sambamba na kuwazuia wanachama wake walioshinda nafasi za uwakilishi visiwani humo, kuapishwa.
“Katika mwaka 2015, nilipoingia rasmi kuwa rais na baada ya uchaguzi Zanzibar kufanyika ule wa marudio, Maalim Seif aliniandikia barua akiniomba kuja kuniona. Nilisita kidogo kwamba kwa nini anataka kuja kuniona na wakati hata kwenye uchaguzi hakushiriki,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amesema, baadae aliamua kuonana na Hayati Maalim Seif.
“Maalim Seif akaandika tena barua ya pili na baadae akaandika ya tatu, kila nilipokuwa nikijaribu kupata ushauri kutoka Zanzibar, nilikuwa naambiwa subiri tu, muache kwanza. Lakini baadaye siku moja niliamua, ngoja nimuone Maalim Seif,” amesema Rais Magufuli.
Amesema, baada ya kuonana na Maalim Seif, “niligundua kwamba alikuwa ni mtu mzuri sana, kiongozi wa tofauti sana. Alipokuja Ikulu Dar es Salaam, nilipoanza kuzungumza nae, nilimuona mtu tofauti sana, tofauti na picha ilivyokuwa imejengeka.”
Rais Magufuli amesema “…sababu mazungumzo yetu yalikuwa mazuri sana na akanieleza, sikushiriki uchaguzi wa pili lakini nataka kukuhakikishia Zanzibar itakuwa salama.”
“Na pia, alimhakikishia kuwa atatoa ushirikiano kwa Rais aliyeko madarakani wakati huo, Dk. Ali Mohamed Shein.”
“Maalim Seif alisema, sitahamasisha fujo yoyote kwa miaka yote mitano, aliyechaguliwa ataendelea kutawala, kauli hiyo niliiona mpaka miaka mitano,” amesema Rais Magufuli.
Akielezea zaidi mazungumzo yake na Hayati Maalim Seif, Rais Magufuli amesema “alisema yeye anapenda amani, angependa Zanzibar na Watanzania wote wakae kwa amani, kauli hiyo aliithibitisha kwa vitendo.”
Rais Magufuli amesema, baada ya mazungumzo hayo, Hayati Maalim Seif alishiriki Uchaguzi Mkuu wa 2020 katika nafasi ya Urais wa Zanzibar, kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, kisha alikubali kushiriki Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo (SUK).
Rais Magufuli amesema, Hayati Maalim Seif alikwenda kijijini kwao Chato mkoani Geita, baada ya kukubali kuunda SUK na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi.
“Ulipotokea uchaguzi Maalim alishiriki, na mara ya mwisho alikuja mpaka Chato na Rais Mwinyi. Alivyokuja kule mazungumzo yake yalikuwa ya raha sana, akanipa historia nzuri yeye akiwa CCM na wakati huo akiwa TANU,” amesema Rais Magufuli na kuongeza.
“Aliniambia aliwahi fika Chato kuhamasisha TANU, na siku zote alikuwa anahubiri umoja wa Zanzibar na Tanzania, kitu ambacho amemaliza nacho.”
Waliovaaa barakoa asanteni kwa kuonyesha mfano, pamoja na Mzee Kikwete……. “ongeza na za kwako”