May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli asamehe wafungwa, mahabusu 1,787 wa Ethiopia

Baadhi ya wahamiaji haramu wa Ethiopia waliowahi kushikiriwa nchini

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, John Pombe Magufuli, ametangaza msahama wa wafungwa na mahabusu 1,789 wa Ethiopia wanaoshikiliwa katika mahabusu na magereza mbalimbali nchini humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Chato … (endelea).

Wafungwa na mahabusu hao, walikamatwa na kukutwa na hatia ya kuingia nchini humo kinyume cha sheria huku akiiruhusu Ethiopia kutuma ndege wakati wowote ili kuwarejesha nyumbani kwao.

Rais Magufuli alitoa msamaha huo jana Jumatatu tarehe 25 Januari 2021, mara baada ya kumaliza mazungumzo na Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde yaliyofanyika nyumbani kwake, Chato mkoani Geita.

Rais Zewde, alikuwa Tanzania katika ziara ya kikazi ya siku moja.

Baada ya mazungumzo yao, Marais hao, walizungumza na waandishi wa habari ambapo, Rais Magufuli amemshukuru Rais Sahle-Work Zewde kwa kufanya ziara nchini humo.

Rais John Magufuli

Alisema, hii inaimarisha na kukuza zaidi uhusiano wa Tanzania na Ethiopia ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mtawala wa Ethiopia, Hayati Haile Selassie I tangu mwaka 1963.

Rais Magufuli alisema, wamezungumzia kukuza zaidi ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji ambao kwa sasa bado upo katika kiwango cha chini licha ya kuwepo ongezeko la biashara kutoka Sh.3.07 bilioni mwaka 2016 hadi kufikia Sh.13.55 bilioni mwaka 2019/20.

Alisema kuna uwekezaji wa miradi 13 ya Ethiopia yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 14.57 iliyozalisha ajira 567 hapa nchini.

Maeneo mengine waliyozungumza ni kuimarisha ushirikiano katika usafiri wa anga na utalii, ulinzi na kupeleka walimu wa kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Ethiopia.

Pia, kushirikiana mbinu za kunufaika na mazao ya mifugo hasa ikizingatiwa Ethiopia na Tanzania zinashikana nafasi ya kwanza na ya pili (mtawalia) kwa idadi kubwa ya mifugo Barani Afrika na kuhakikisha Kamati ya Pamoja ya Majadiliano (JPC) inakutana haraka ili kupitia maeneo yote ya ushirikiano na kuongeza maeneo mapya.

Rais wa Ethiopia, Sahle-Work Zewde

Kuhusu viwanja vya Tanzania vilivyopo Addis Ababa ambavyo Serikali ya Ethiopia ilivinyang’anya kutokana na Tanzania kutoviendeleza kwa mujibu wa sheria za Ethiopia, Rais Magufuli alisema Serikali ya Tanzania imechukua hatua dhidi ya waliohusika katika upotevu wa fedha za uendelezaji wa viwanja hivyo na ameiomba Serikali ya Ethiopia kuvirejesha kwa Tanzania ili viendelezwe.

Kwa upande wake, Rais Sahle-Work Zewde alimshukuru Rais Magufuli kwa kumkaribisha na alishukuru kwa kuendeleza uhusiano mzuri wa Tanzania na Ethiopia uliodumu tangu enzi za kupigania ukombozi wa Afrika.

Alimpongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kwa kipindi cha pili kuiongoza Tanzania na amebainisha Ethiopia ipo tayari kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania hususani kukuza biashara na uwekezaji.

Rais  Sahle-Work Zewde alisema Tanzania ni nchi muhimu Barani Afrika kutokana na kuhusika kwake katika masuala ya kimajumuhi ikiwemo kutafuta amani na ndio maana Ethiopia ipo tayari wakati wote kushirikiana na Tanzania.

Alipokea ombi la kurejeshwa kwa viwanja vya Tanzania vilivyonyang’anywa na Serikali ya Ethiopia kutokana na kutoendelezwa, ameshukuru kwa utayari wa Tanzania kupeleka walimu wa kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Ethiopia, ameafiki ushirikiano wa Tanzania na Ethiopia katika kunufaika na utajiri wa mifugo mingi iliyopo na ameishukuru Tanzania kwa utayari wake wa kuwaachia wafungwa na maabusu wa Ethiopia 1,789 waliopo magerezani hapa nchini baada ya kukamatwa na kukutwa na hatia ya kuingia nchini kinyume cha sheria.

error: Content is protected !!