July 31, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli apuuza donda la Wazanzibari

Spread the love

RAIS John Magufuli amepuuza maalamiko ya Wazanzibar kwamba, Chama Cha Mapinduzi (CCM) licha ya kukataliwa, kimelazimisha kurudi madarakani, anaandika Mwandishi Wetu.

Amempongeza Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), kwa kile alichosema “ametimiza wajibu wake wa kusimamia uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka jana vizuri.”

Kwa kauli hiyo ambayo Dk. Magufuli ameitoa leo kwenye hafla ya kukabidhiwa ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania uliofanyika mwaka jana, hajabadilisha msimamo kuhusu mgogoro wa kisiasa Zanzibar uliotokana na uchaguzi huo.

Rais Magufuli amesema, uamuzi alioufanya wa kupeleka Zanzibar askari wengi wa vikosi vya ulinzi na usalama kulinda ili uchaguzi wa marudio wa 20 Machi 2016 uwe wa amani na salama ulikuwa sahihi na kwamba, naye alitimiza jukumu lake kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema, hakuna uchaguzi unaokosa kasoro hata ndogo lakini anashangaa kwamba, wapo watu wanahangaika mpaka nje ya nchi kuieleza vibaya serikali kwa kuwa, nilisema siwezi kuingilia tume ambayo ni huru.

“Ni kweli sina mamlaka ya kuingia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ambayo ikifanya uamuzi haiwezi kuhojiwa lakini nilipochukua hatua za kuimarisha ulinzi, nilitimiza wajibu wangu,” amesema.

Hata hivyo amesema kwa kurudia kuwa, uchaguzi umwekwisha nchini na sasa ni wakati wa kuwatumikia wananchi katika maendeleo.

“Walewale waliokuja kunitaka niingilie maamuzi ya tume nikakataa wamekuwa wanaisema serikali ninayoongoza,” amesema bila kutajia jina la mtu huyo lakini alikuwa akimlenga Maalim Seif Sharif Hamada, Katibu Mkuu wa CUF.

Maalim Seif yupo ziarani nchini Marekani, Canada ambapo amekuwa akieleza hali halisi ya uchaguzi wa Zanzibar namna ulivyovurugwa na Serikali ya CCM kwa lengo la kuendelea kubaki madarakani.

CUF chini ya Maalim Seif anayejinasibu kuwa ndiye rais wa Zanzibar aliyechaguliwa kihalali na wananchi, kinapinga uamuzi wa Jecha kufuta uchaguzi uliofanyika Zanzibar tarehe 25 Oktoba 2015 kwa kuwa, hakuwa na mamlaka ya kisheria ya kufanya hivyo.

Jecha alifuta uchaguzi huo tarehe 28 Oktoba 2015 kwa madai uliharibika na kisha kusimamia ualioitwa uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi 2016.

Baada ya uchaguzi huo Jecha alimtangaza Dk. Shein, mgombea wa CCM kuwa mshindi wa urais.

error: Content is protected !!