August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli aonywa kero za Muungano

Mariam Msabaha, Mbunge wa Viti maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)

Spread the love

MARIAM Msabaha, Mbunge wa Viti maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar amemtaka Rais John Magufuli kuangalia upya changamoto za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, anaandika Pendo Omary.

Katika mahojiano aliyofanya na MwanaHALISI Online, Mariam amesema, “Marais wote waliopita walijua Zanzibar ina matatizo, walikuwa wanakaa chini wanazungumza. Hakuna kitu kibaya kama watu kukaa hamsikilizani. Zanzibar ni ndogo sana. Sijui hili suala la Muungano, Rais Magufuli kaliweka wapi.

“Chama cha Wananchi – CUF ndicho chama chenye nguvu Zanzibar. Huo ndiyo ukweli. Kama mwanzo walikaa na Chama Cha Mapinduzi wakaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), nini kinashindikana sasa hivi?”

Amesema kuwa tambo za serikali zote mbili chini ya CCM, Bara na Visiwani kuwa zimepunguza kero za Muungano hazina mashiko kwani kero nyingi bado hazijatatuliwa ipasavyo huku akitoa mfano wa malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu vikwazo wanavyotaka kuingiza bidhaa Tanzania Bara kutoka Zanzibar.

“Tatizo hili haliwaathiri tu wafanyabiasahara wa Zanzibar bali hata wafanyabiashara wa upande wa Tanzania Bara ambao hufika Zanzibar kununua bidhaa mbalimbali kwani wamekuwa wakitozwa kodi, jambo linalomuongezea mzigo wa gharama mnunuzi.

“Sasa hivi Mtanzania kutoka Bara akienda Zanzibar kununua gari na kutaka kusafirisha si rahisi kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma kwasababu njia imejaa vikwazo ambavyo ni wachache wanaweza kuvimudu na vinachangia mdororo wa kiuchumi kwa kiasi kikubwa,” amesema Mariam.

error: Content is protected !!