December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli aongoza Watanzania kumuaga Balozi Kijazi

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, John Magufuli, amewaongoza waombolezaji, kuuaga mwili wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi (64), aliyefariki dunia tarehe 17 Februari 2021, Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma. Anariporti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Shughuli ya kuuaga mwili wa Balozi Kijazi, imefanyika leo Ijumaa tarehe 19 Februari 2021, viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam na kuhudhuliwa na viongozi mbalimbali wa kiserikali, Bunge na mahakama.

Ibada ya mazishi ya kuaga mwili Balozi Kijazi, imeongozwa na Padre Joseph Matumain, Paroko wa Kanisa Kuu Katoliki la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Katika mahubiri yake, Padre Matumain amesema, Balozi Kijazi “alifanya kazi kubwa sana katika taifa letu. Tunamwombea ili mwenyezi Mungu aweze kumsaheme.”

“Sisi tuliobaki, tunapaswa kujiandaa ili wakati wowote, tukiitwa tuwe tayari na kujitayarisha kwa matendo yetu,” amesema Padre Matumaini.

Viongozi wengine waliohudhulia ni; Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete; Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan; Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu; Profesa Ibrahim Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla

Pia, mawaziri, makatibu wakuu wa wizara mbalimbali, wakuu wa taasisi binafsi na za umma na viongizo wa kisiasa akiwemo, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally wameshiriki mazishi hayo.

Mwili wa Balozi Kijazi aliyezaliwa tarehe 18 Novemba 1956, utazikwa kesho Jumamosi nyumbani kwao, Korogwe jijini Tanga.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online na MwanaHALISI TV kwa habari mbalimbali

error: Content is protected !!