Monday , 22 April 2024
Habari za Siasa

Magufuli anashitakika

John Magufuli, Rais wa Tanzania
Spread the love

RAIS John Magufuli, anaweza kushitakiwa kwa makosa aliyoyatenda wakati akiwa waziri wa Ujenzi katika serikali ya Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, anaandika Saed Kubenea.

Hii ni kwa kuwa kinga iliyotajwa kwenye Ibara Katiba ya Jamhuri ya Muungano kwa rais kutoshitakiwa, haizungumzii makosa ambayo kiongozi huyo alitenda kabla ya kuwa rais.

Kwa mujibu wa Ibara ya 46 (2) ya Katiba, rais anaweza kushitakiwa kwa kupewa “taarifa siku 30 kabla ya shauri kufunguliwa mahakamani au atakuwa ametumiwa kwanza taarifa ya madai kwa maandishi….”

Taarifa ndani ya serikali zinasema, kati ya mwaka 2002 na 2005, Magufuli akiwa waziri wa ujenzi, anadaiwa kuwa aliamuru kuvunjwa kwa mkataba wa ujenzi kati ya serikali na kampuni ya Stirling Civil Engineering Limited (SCEL), kutoka nchini Canada.

Kufuatia uamuzi huo wa serikali, inaelezwa kuwa kampuni hiyo ya kigeni ilikimbilia mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya kibiashara, ambako serikali ya Tanzania imeamriwa kulipa kiasi cha dola za Marekani 38.7 milioni (Sh. 87 bilioni).

Mkataba uliovunjwa na ambao ni chanzo cha deni, ulikuwa Na.10050/98/99 uliopewa jina la “Bagamoyo Project – Dar es Salaam (Wazo Hill).”

Aidha, kufuatia uamuzi huo, kampuni ya Canada imeamua kushikilia ndege ya Tanzania – Bombadier Q400 – na kutoa masharti mazito kwa Rais Magufuli juu ya deni lake.

SCEL imesema katika barua yake kwa Rais Magufuli, “iwapo serikali itashindwa kulipa kiasi hicho, kampuni tutaitapiga mnada ndege tuliyoishikilia.”

Tayari kampuni ya mawakili ya Irving Mitchell Kilichman (IMK) – kwa niaba ya kampuni ya SCEL inayoshikilia ndege ya Tanzania – imemwandikia barua Rais Magufuli, ikimuonya kutekeleza makubaliano mapya iliyofunga na serikali yake.

Barua kutoka IMK imenakiliwa kwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Dk. Augustine Mahiga na Balozi wa Tanzania nchini Canada, Jack Mugendi Zoka.

Katika barua hiyo ya tarehe 4 Agosti 2017, wadai (SCEL) wanarejea mazungumzo kati yao na ujumbe wa serikali ulioshirikisha Dk. Mahiga na Balozi Zoka.

SCEL inasema katika barua kwa Rais Magufuli, “gharama hizi zinafuatia kuvunjwa kwa mkataba kati ya kampuni ya na serikali ya Tanzania. Mahakama iliidhinisha kiasi cha dola za Marekani 25 milioni na riba ya asilimia nane (8%) hadi deni litakapolipwa.”

Siku moja baadaye, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kilitoa tamko katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu sakata hilo.

Mkutano ulihutubiwa na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, akiambatana na viongozi waandamizi wa chama hicho.

Lissu alisema ndege ya Bombadier iliyokuwa iwasilishwe nchini mwezi mmoja uliopita, ilikamatwa na kampuni ambayo mkataba wake wa ujenzi wa barabara ulikatishwa wakati Rais Magufuli alipokuwa waziri wa ujenzi – mwaka 2009.

Lissu alieleza kuwa tarehe 10 Desemba, 2009 kampuni ya SCEL ilifungua mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi; na tarehe 10 Juni 2010 mahakama ilitoa tuzo ya dola za Marekani milioni 25 na riba ya asilimia nane (8%) kila mwaka hadi malipo yatakapofanyika.

“Tuzo hiyo imesajiliwa na kutambuliwa kama deni halali la Serikali ya Tanzania kwa SCEL katika nchi za Ufaransa, Uholanzi, Ubelgiji, Uingereza na Uganda,” ameelerza Lissu.

Wakili huyo amesema hadi sasa Serikali ya Tanzania haijalipa deni hilo ambalo sasa, kutokana na kuongezeka kwa riba, limeongezeka hadi dola 38,711,479 kufikia tarehe 30 Juni mwaka huu.

“Hapo ndipo SCEL ilipoamua kuomba amri ya Mahakama Kuu ya Montreal ya kukamata mali zote za Tanzania zilizopo kwa kampuni ya Bombardier, zikijumuisha ndege ya Bombardier Q400,” ameeleza Lissu.

Katika mazungumzo kati ya serikali na kampuni hiyo, tarehe 3 mwaka huu, ilikubaliwa kuwa ndege hiyo itaachiliwa iwapo serikali italipa kwanza dola milioni 12.5.

Baada ya hapo SCEL itafuatilia mazungumzo kwa kutuma ujumbe Tanzania kwa ajili ya kuwekeana utaratibu wa kukusanya kiasi kilichosalia.

Kwa mujibu wa barua kwa rais, pande zote mbili zilikuwa zimekubaliana awali kuwa suala hili libaki kuwa siri hadi malipo yatakapokuwa yamefanyika. Haikuwa hivyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Samia aridhishwa utendaji mabalozi, awapa neno

Spread the loveRais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amewapongeza mabalozi  wanaowakilisha ...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NMB yadhamini Mkutano Mkuu ALAT, kufunguliwa na Samia

Spread the loveBENKI ya NMB, imekabidhi hundi yenye thamani ya Sh. 120...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mipango na uwekezaji kutumia bilioni 121.3, mradi wa Bagamoyo wapewa kipaumbele

Spread the loveWIZARA ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, imeliomba Bunge...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mbunge ataka kasi uzalishaji walimu ipunguzwe akidai hakuna ajira

Spread the loveMBUNGE wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, ameishauri Serikali ipunguze kasi...

error: Content is protected !!