June 16, 2021

Uhuru hauna Mipaka

‘Magufuli anasafiria nyota ya Kikwete’

Spread the love

LICHA ya Serikali ya Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete kutuama katika tuhuma ya uzembe, ufisadi na rushwa, sehemu ya utawala wake unatajwa kumbeba Rais John Magufuli, anaandika Regina Mkonde.

Hatua ya Serikali ya Rais Magufuli kupunguza bei ya umeme inatajwa kuandaliwa na mtangulizi wake Rais Kikwete na kwamba, miundombinu Shirika la Umeme nchini (Tanesco) na mingine iliyoandaliwa na mtangulizi wake, inamsaidia kuinua uchumi wa nchi.

Serikali jana imetangaza kupunguza bei ya umeme pia kuondoa kodi ya huduma kwa mwezi Sh. 5520 hatua ambayo imepokelewa kwa mikono miwili na wananchi huku baadhi ya wachambuzi wakieleza kuwa, hatua hiyo haitoleta mabadiliko kwenye uchumi wa nchi kulingana na asilimia ndogo ya mabadiliko katika bei.

Akizungumza na MwanaHALISI Online Bashiru Ally, Mhadhiriwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) amesema, mafanikio hayo si ya Rais Magufuli isipokuwa ni ya mtangulizi wake.

“Ni vigumu kusema kuwa anachofanya rais ni jitihada zake na kwamba Rais Kikwete hakufanya kitu, tusisahau kuwa miradi mingi ya umeme na miundombinu ilijengwa na Rais Kikwete,” amesema Bashiru na kuongeza;

“Huyu amekuja kuanzia sehemu aliyoishia mtangulizi wake na yeye ataacha misingi na changamoto ambazo zitakuja kutatuliwa na anayefuata.”

Hata hivyo, Bashiru amepongeza hatua hiyo kwa kuwa, katika hali fulani itawasaidia wananchi kupunguza makali ya maisha hasa wajasiliamali wadogo wanaotegemea kuingiza mapato kupitia nishati ya umeme.

“Wazalishaji watanufaika baada ya kushuka kwa bei ya umeme, kutasaidia kupunguza mfumuko wa bei nchini kama unavyopanda wakati gharama za umeme zinapopanda,” amesema Bashiru.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi nchini, Profesa Ibrahim Lipumba amesema kwamba, Rais Magufuli bado hafikia viwango vya kukomboa uchumi wa nchi.

Amesema, hatua ya kushusha bei ya umeme haijafikia kiwango cha kusaidia uchumi wa nchi kama ambavyo baadhi ya watu wanavyoweza kudhani.

“Ukitazama kwa ndani utaona kwamba hakuna mshuko mkubwa wa bei ya umeme iliyofanyika ukilinganisha na kushuka kwa bei ya petrol kulikotokea mwaka jana, sababu bei ya Petrol mwaka 2015 ilishuka sana na kufikia nusu ya bei iliyokuwa ikiuzwa,” amesema Prof. Lipumba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF).

Ameeleza kuwa kama bei ya umeme ingeshuka kwa asilimia 20 ingesaidia kuimarisha uchumi wa wananchi hasa wale wenye viwanda vidogo.

“Iwapo bei ingeshuka kwa asilimia 20 ingesaidia kujenga uchumi wa nchi kwa asilimia kubwa pia kungekuwa na umeme wa uhakika hali ambayo ingesaidia kuimarisha uchumi,” amesema Prof. Lipumba.

Akizungumzia kuhusu Tanzania kunyimwa misaada na Mfuko wa Chanagamoto za Milenia (MCC), Profesa huyo ametoa wito kwa serikali kurejesha misingi mizuri ya demokrasia na kujenga uaminifu duniani kote kulingana na namna ilivyojinasibu kuwa nchi inayoendeshwa kwa misingi ya demokrasia na uhuru.

“Wahisani waliamua kufuta misaada yao baada ya kuona uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu visiwani Zanzibar haukufuata demokrasia hali iliyotafsiriwa na wahisani kama kwenda kinyume na makubaliano baina yao na MCC,” amesema.

Anasema Tanzania iliingia mkataba na MCC na ikasaini makubaliano ya kuendeleza misingi ya demokrasia na haki na ndiyo sababu ya kukubaliwa kupewa msaada wa Sh. 360 Bilioni ambazo zimezuiliwa.

Prof. Lipumba anafafanua kwamba fedha hizo zililenga kuwekeza kwenye sekta ya nishati ili nchi ipate umeme wa uhakika utakaokidhi mahitaji ya viwanda hivyo kutopatikana kwa fedha hizo kuna athiri uchumi wa nchi.

Prof. Benson Bana, Mhadhiriwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema, kushuka kwa bei ya umeme kutasaidia kupunguza mfumuko wa bei.

“Umeme unatumika kwa wingi viwandani hivyo kushuka kwa gharama za umeme kutasaidia kupungua kwa mfumuko wa bei,” amesema Prof. Bana.

Kuhusu kukatishiwa misaada na nchi wahisani, amesema serikali haina budi kuangalia upya sera ya urafiki na diplomasia ya nchi za nje.

“Kuna baadhi ya maeneo yataathirika hivyo lazima serikali ijitahidi kubana matumizi mahali Fulani ili kuziba pengo hilo,” amesema Bana.

Amesema ingawa kujenga uchumi wa nchi itachukua muda lakini baadaye mambo yatakaa sawa na hata vizazi vijavyo vitanufaika na kuishi kwa raha kama wanavyoishi raia wa nchi nyingine.

error: Content is protected !!