Monday , 26 February 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Magufuli amtolea nje Mkapa
Habari za SiasaTangulizi

Magufuli amtolea nje Mkapa

Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa (kushoto) akiteta jambo na Rais wa Tanzania, John Magufuli
Spread the love

JOHN Pombe Magufuli, mwenyekiti wa taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), “amegoma” kutekeleza ushauri wa rais mstaafu, Benjamin Mkapa, MwanaHALISI Online limeelezwa…(endelea).

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho tawala zinasema, Mkapa alimtaka Rais Magufuli, kufanya mabadiliko ya uongozi wa juu wa chama chake kwa kuwapumzisha baadhi ya viongozi wandamizi na kuingiza damu mpya.

Miongoni mwa waliotakiwa kupumzishwa, ni makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tanzania Bara, Philiph Mangula. Mwingine aliyetakiwa kupumzishwa, ni katibu mkuu wake, Abdulrahaman Kinana.

Mkapa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa miaka 10, alimtaka Magufuli kumpimzisha Mangula, kwa maelezo kuwa tayari amezeeka na hivyo angeweza kukisaidia chama hicho kwa ushauri akiwa nje ya uongozi.

Kwa upande wa Kinana, mtoa taarifa anasema, rais huyo mstaafu wa awamu ya tatu, alimtaka Magufuli kumkabidhi wadhifa wa makamu mwenyekiti Bara.

“Mzee Mkapa alimtaka mwenyekiti wake wa taifa (Rais John Magufuli), kumpumzisha Magula kwenye nafasi ya makamu mwenyekiti Bara. Alisema, Magula ameshazeeka na hivyo hawezi kukisaidia chama hicho akiwa ndani ya uongozi,” anaeleza mtoa taarifa wa MwanaHALISI Online..

Anasema, “Mzee Mangula angeweza kusaidia sana chama kama angekuwa mshauri; anayetoa ushauri wake nje ya jukwaa la uongozi.

“Akamtaka pia kumbadilishia majukumu Kinana kwa kumtoa kwenye nafasi ya katibu mkuu na kumkabidhi nafasi ya makamu mwenyekiti kwa sababu zilezile za umri.”

Anasema, “lakini mwenyekiti (Rais Magufuli), amegoma. Amemrudisha Mzee Mangula kwenye nafasi yake. Akamuacha Kinana kuendelea kuwa katibu mkuu na akabakisha sekretarieti yote ya chama kuendelea na majukumu yake kama ilivyokuwa. Haifahamiki kwa nini amekataa ushauri huo.”

Anaongeza, “yawezekana anapeleka ujumbe kuwa anataka kuwa huru katika kuendesha chama na serikali. Kwa maneno mengine, pengine hataki kuingiliwa katika utendaji wake wa kazi.”

Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja wiki moja tokea aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba, kuhutubia mkutano mkuu wa CCM mjini Dodoma na kumsifu kiongozi huyo kuwa amekuwa anasimamia bila woga kile anachokiamini.

Makamba ambaye alikuwa katibu mkuu wa CCM kati ya mwaka 2006 hadi 2011, aliuambia mkutano huo mkuu kuwa aliwahi kutoa ushauri kwa mwenyekiti wake huyo juu ya uendeshaji wa chama, lakini aligoma kuutekeleza.

Alisema, “kuna siku nilikutumia meseji ukaniambia ushauri mbovu huutaki, hivyo ndivyo inavyotakiwa mimi sikukasirika. Kazi yetu sisi tuliowahi kuwa wajumbe wa Kamati Kuu (CC), ni kukushauri.”

Alisema, “kuna baadhi ya watu wamekuwa wakisema, sisi tuliowahi kuwa viongozi wa chama hiki, hatutaki kukushauri. Napenda kusema, hilo siyo kweli.”

Makamba ambaye ni hodari katika uzungumzaji wa kutumia vitabu vya dini aliamsha shangwe aliposema, “…mimi niliwahi kukushauri. Ukaniambia Mzee Makamba, ushauri wako nimeusikia, lakini sitaupokea kwa kuwa ni ushauri mbovu.”

Alisema, “tunakufahamu kuwa wewe una uwezo mkubwa wa kazi ya urais na ndiyo maana Kamati Kuu, ilipokutana ikakupendekeza. Unastahili kuwa mwenyekiti wa CCM kwa kuwa moja ya matatizo tunayoyapata ndani ya CCM ni watu kutosema ukweli, wanageuza matatizo, fitina ndiyo ukweli.”

Alisema, “nilipotoa ushauri wangu na haukupokelewa, mimi sikukasirika…kazi yetu ni kushauri…mtekelezaji ni wewe.”

Makamba alitoa kauli hiyo, wakati akitoa salamu kwa wajumbe wa mkutano mkuu. Alisifu msimamo wa mwenyekiti wake, kwa maelezo kuwa amekuwa akisimamia yale anayoaamini bila woga ikiwamo kukataa ushauri ambao anaona hauna tija.

Hata hivyo, akiongea mithili ya mtu mwenye donge moyoni, Makamba alisema, “…mwenye uwezo wa kusema wapumbavu ni Mkapa. Mzee Mwinyi hawezi kwa kuwa ni muungwana. Kikwete hawezi kwa kuwa ni muungwana na mimi siwezi kwa kuwa ni muungwana.”

Kwa mujibu wa taarifa hizo, katika mabadiliko yaliyopendekezwa na Mkapa, aliyepata kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ndiye aliyependekezwa kuwa katibu mkuu.

“Katika mabadiliko ambayo Mzee Mkapa alimfikishia Rais Magufuli, Nape ndiye aliyependekezwa kuchukua nafasi ambayo ingeachwa wazi na Kinana,” anaeleza mtoa taarifa.

Nape na Kinana, walizunguka nchi mara kadhaa kufufua CCM na kukiandaa kwa ushindi katika uchaguzi wa 2015.

Hata hivyo, katika siku za karibuni, mwanasiasa huyo amegeuka kuwa mkosoaji mkubwa wa utendaji wa serikali ya Rais Magufuli bungeni tangu alipondolewa kwenye wazifa wa uwaziri, Machi mwaka huu.

Mbunge huyo wa Mtama, analalamikiwa kwa kauli zake tatu‎ alizozitoa hivi karibuni, kuwa zimekuwa mwiba kwa serikali ya Rais Magufuli, jambo ambalo lilisababisha kuwapo kwa tishio la kumuita kwenye kamati ya maadili kumhoji.

Miongoni mwa kauli zake hizo, ni ile aliyoitoa muda mfupi baada ya kutenguliwa uteuzi na kutaka kuzungumza na waandishi wa habari, ambapo alizuiliwa na polisi.

Hapa Nape alisema, “nchi hii ni yetu sote, tuungane kumpinga yoyote anayetaka kutuvuruga. Mimi ni mtu mdogo sana ndani ya Tanzania, Nape hawezi kuwa mkubwa kuliko Tanzania. Lakini kamwe tusikubali mtu yeyote kutuvugia amani na mshikamano wetu kwa maslahi yake binafisi.”

Katika mkutano huo, Nape alionyeshwa kushangazwa na kitendo cha polisi kumnyooshea bunduki alipokuwa akitaka kuzungumza na wanahabari katika eneo hilo.

Akiwa na jazba za kuzuiwa kuzungumza na wanahabari, Nape alihoji polisi waliomzuia kuzungumza huku wakiwa na bastola kwamba nani amewatuma.

Alisema, yeye amekitoa chama hicho shimoni kwa kuzunguka nchi nz‎ima na wakati akifanya hivyo wao na aliowatuma, walikuwa mjini wakistarehe.

Mkutano kati ya Nape na waandishi ulipangwa kufanyika katika hoteli ya Protea, jijini Dar es Salaam, tarehe 23 Machi mwaka huu.

Akijibu kauli ya Nape, mrithi wake kwenye nafasi hiyo ndani ya chama hicho, Hamfrey Polepole, alinukuliwa akisema, chama chake hakiwezi kuvumilia kauli zinazotolewa na Nape.

Polepole alisema, “ni lazima tutamhoji Nape, kuhusiana na kauli yake kwamba ameitoa CCM shimoni. Yeye nani mpaka akitoe chama hiki shimoni? Tutamuita ili atueleze. Hatuwezi kuruihusu chama hiki kinadhalilishwa kwa kiwango hiki.”

Tangu wakati huo, taarifa zinaeleza, Nape amekuwa hana uhusiano mzuri na baadhi ya viongozi wakuu ndani ya chama na serikali.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Hamahama Ngorongoro kutikisa maandamano ya Chadema Arusha

Spread the loveMAELFU ya wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na...

Habari za SiasaTangulizi

Waliofariki ajalini Arusha kuagwa siku ya maandamano Chadema

Spread the loveMIILI ya watu 25 waliofariki dunia katika ajali iliyohusisha lori...

Habari za SiasaTangulizi

Serikali kuiburuzwa mahakamani ajali iliyoua 25 Arusha

Spread the loveMTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), imeitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Samia atoa pole ajali iliyoua 25, kujeruhi 21 Arusha

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu...

error: Content is protected !!