July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli amteua Mahadhi balozi Kuwait

Spread the love

MWANASHERIA na muandishi wa habari aliyeingia katika siasa miaka ya 2000, Mahadhi Juma Maalim, ametuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kuwait kuanzia leo. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Mahadhi ameteuliwa katika uteuzi mpya uliofanywa na Rais John Magufuli leo akimpa nafasi mpya baada ya kuwa naibu waziri kwa miaka kumi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akianzia kwa Dk. Asha-Rose Migiro na kumalizia kwa Bernard Membe.

Mahadhi alianza kusomea uandishi wa habari na kufanya kazi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, akiwa gazeti la Nuru, ambalo baadaye lilibadilishwa jina na kuitwa Zanzibar Leo, na baadaye kusoma shahada ya sheria nchini Australia.

Alipoingia kwenye siasa, aligombea ubunge jimbo la Muyuni, Mkoa wa Kusini Unguja, na kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu wa 2005. Aligombea tena nafasi hiyo uchaguzi wa mwaka 2010 akashinda.

Kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka jana 2015, Mahadhi alishindwa katika kura za maoni na kubaki mmoja wa mawaziri wa mstaafu Rais Kikwete walioangushwa uchaguzini.

Uteuzi wake unakwenda sambamba na agizo la Rais Magufuli kutaka mabalozi Dk. Batilda Salha Burian aliyekuwa Japan na Dk. James Msekela aliyekuwa Italia, wakabidhi ofisi kwa maofisa wasaidizi baada ya mikataba yao ya kazi kumaliza muda.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Peter Kallaghe.

Kwa maana hiyo, kwa sasa inatarajiwa Rais Magufuli kulazimika kuteua mabalozi wapya wa nchi hizo, pamoja na Ubelgiji ambako aliyekuwa Balozi, Dk. Deodorous Kamala kuchaguliwa mbunge, na nchini Malyasia ambako alikuweko Dk. Aziz Mlima ambaye ameteuliwa kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Magufuli amewaondoa Balozi Burian na Msekela kwa sababu wamekuwa hawafanyi kazi vizuri.

error: Content is protected !!