August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli amtambua Lipumba, Jecha awa kivutio

Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF)

Spread the love

RAIS John Magufuli, amemtaja Prof. Ibrahim Lipumba kama miongoni mwa viongozi wa vyama vya siasa waliohudhuria sherehe za Uhuru zilizofanyika siku ya leo jijini Dar es Salaam, anaandika Charles William.

Kitendo hicho cha Rais Magufuli kimezua gumzo kutokana na mvutano unaoendelea ndani ya Chama Cha Wananchi – CUF ambapo Baraza Kuu la chama hicho lina msimamo wa kutomtambua Prof. Lipumba kama kiongozi wao huku pia likiwa limetangaza kumvua uanachama wa CUF.

“Napenda nitambue uwepo wa viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa hapa nchini, Profesa Lipumba na wengineo nawashukuru wote sana kwa kujitokeza katika sherehe hizi,” amesema Rais Magufu katika utangulizi wa hotuba yake.

Prof. Lipumba amekuwa katika mvutano na CUF kufuatia hatua yake ya kujiuzulu uongozi wa chama hicho Agosti mwaka jana kisha kutangaza kutengua kujiuzulu kwake mwezi Juni mwaka huu, huku Jaji Francis Mutungi ambaye ni Msajili wa Vyama vya Siasa hapa nchini akitoa msimamo wa kumtambua kama mwenyekiti wa CUF Taifa.

Hatua hiyo ilisababisha wafuasi na viongozi wanaoumuunga mkono Prof. Lipumba kuvamia ofisi kuu ya chama hicho eneo la Buguruni na kuishikilia huku viongozi wasiomuunga mkono wakiondoka na sasa chama hicho kimefungua kesi dhidi ya msajili na Lipumba.

CUF kwa sasa imetengaza kuwa chini ya uongozi wa Julius Mtatiro ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi mpaka mwaka 2019 ambapo uchaguzi mkuu wa chama hicho utafanyika.

Prof. Lipumba naye amekuwa akijitambulisha kama mwenyekiti halali wa chama hicho huku akikupambana na upinzani mkali katika ziara za kukagua uhai wa chama hicho mikoani kiasi cha Jeshi la Polisi kulazimika kumpa ulinzi huku likizuia Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF kufanya ziara kama hizo.

Hatua ya Rais Magufuli kumtaja leo katika uwanja wa Uhuru kama kiongozi wa chama cha siasa imekoleza mjadala juu ya watu wanaomuunga mkono na kumtambua Prof. Lipumba huku ruzuku ya CUF ikiwa imezuiliwa kwa muda mpaka pale mvutano ndani ya chama hicho utakapomalizika.

Katika hatua nyingine, Jecha Salim Jecha, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Visiwani Zanzibar (ZEC) alikuwa kivutio kikubwa katika sherehe hizo za Uhuru ambapo alikuwa miongoni mwa viongozi mashuhuri walioketi jukwaa maalum la viongozi.

Viongozi wengi walionekana kumsalimu kwa bashasha huku mwenyewe akionekana mwenye furaha tele. Jecha alijipatia umaarufu mkubwa mara baada ya kutangaza kufuta uchaguzi mkuu Zanzibar kwa madai kuwa haukuwa huru na wa haki.

Tangazo la Jecha lilitolewa kupitia televisheni ya Zanzibar (ZBC) wakati huo Maalim Seif aliyekuwa mgombea urais kupitia CUF akiwa tayari amejitangaza kuwa mshindi wa uchaguzi huo.

CUF ilisusia marudio ya uchaguzi huo yaliyofanyika tarehe 20 Machi mwaka huu na hivyo CCM kutagazwa kujipatia ushindi wa zaidi ya asilimia 90.

error: Content is protected !!