May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli amsulubu hadharani mbunge Abood

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, John Magufuli ameeleza kutamani mfanyabiashara Rostam Azizi kugombea Jimbo la Morogoro Mjini, ili kumng’oa Abdul-Aziz Abood, mbunge wa jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).

Akizindua Kiwanda cha Ngozi cha Ace Leather, Kihonda mkoani Morogoro leo Ijumaa tarehe 12 Februari 2021, kinachomilikiwa na Rostam, Rais Magufuli ameeleza kukerwa na Abood kushindwa kuendesha viwanda viwili alivyoviomba kutoka serikali hivyo kuwanyima ajira wananchi.

“Nafikiri siku moja uje (Rostam) kugombea ubunge hapa umuondoe huyu aliyewanyima ajira wananchi. Huyo leo simpongezi ingawaje jana nilimpongeza, kwenye viwanda ndugu Aboud hujafanya vizuri,” amesema Rais Magufuli huku akisisitiza “nikiondoka hapa bila kusema haya, nitakuwa mnafiki.”

Amesema, Abood alipewa viwanda viwili; kiwanda cha Moproco na kiwanda cha Canivan mkoani humo, lakini hakuviendeleza na hata kusababisha baadhi ya wapiga kura wake kufa bila kuwa na ajira.

Amesema “Moproco kilikuwa kinahusika na cooking oil (mafuta ya kupikia), mafuta ya mwanzo kutengenezwa yalikuwa yanatengenezwa Moproco hapa, mbunge wetu mimi nakusema hadharani, sikufichi ukapewa hivyo viwanda tangu mwaka 1996 mpaka mwaka jana walipokunyang’anya.”

Rais John Magufuli

“…kwa hiyo ukawanyima ajira hata wapiga kura wako, kwa hiyo inawezekana wengine wamekufa kwa kusoka ajira lakini ukawa unawabeba kwenye magari yako kwenda kuwazika, hongera kwa kuwazika. Huu ndio ukweli na mimi nitabaki siku zote kuzungumza ukweli,” amesema Rais Magufuli.

Amesema, kiwanda kimoja kikauzwa na Benki ya CRDB ambapo nayo (CRDB), wamekaa na kiwanda hicho bila kukiendeleza huku watu wakikosa ajira.

“Nao wamekaa nacho (CRDB), Waziri wa Viwanda na Naibu Waziri nataka CRDB wahakikishe kiwanda kile cha Canivas, eidha wanampa mtu bure ama wanakiendesha,” amesema Rais Magufuli.

Akiziungumzia uwekezaji alioufanya Rostam ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Igunga (CCM), amesema amefanya jambo zuri linalohitaji kupongezwa.

Amemweleza Rostam kuwa, aanzishe viwanda vingine ama achukue hata vile ambavyo vinamilikiwa lakini wamiliki wake hawaviendeleza, akimuhakikishia serikali itamlinda.

“Muanzilishi wa kiwanda hiki Rostam na wengine, tutakulinda tutakulinda. Mimi nataka nyie Watanzania muwe mabilionea.

“Anzisha hata kingine, chukua hata vile ambavyo wamepewa hawaviendelezi…, sio Abood aliyekwenda kukopa CRDB fedha zikaliwa, miaka 24 watu wanakosa ajira. Rostam nakupongeza kwa dhati, unaweza kufanya kosa ukarekebisha kosa,” amesema Rais Mafuguli.

Rais Magufuli amesema, uanzishwaji wa viwanda una faida kubwa, na kwamba malighafu zinapopelekwa nje, watu wa huki ndio wanatengenezewa ajira ya kuchakata hizo malighafi.

error: Content is protected !!