July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli amsafisha Injinia Masauni

Spread the love

YULE mwanasiasa ambaye mwaka 2010 alinyang’anywa uenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kwa kutuhumiwa kugushi umri, ndiye Naibu Waziri mpya wa Mambo ya Ndani. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Hamad Masauni Yussuf, mhandisi, ameteuliwa na Rais Dk. John Magufuli kushika wadhifa wa unaibu waziri akiwa mmoja wa viongozi walioteuliwa jana katika hatua ya Rais kukamilisha uundaji Baraza la Mawaziri.

Injinia Masauni ameteuliwa akiwa Mbunge wa Kikwajuni kwa kipindi cha pili sasa na anaingia katika wizara mojawapo za Muungano, ambazo imezoeleka kuongozwa na mawaziri au manaibu wao kutoka Zanzibar.

Katika kipindi kilichopita, wizara hiyo ilishikwa na Shamsi Vuai Nahodha, baada ya kuteuliwa mbunge na Rais Jakaya Kikwete, baadaye akateuliwa Mathias Chikawe, lakini naibu wake akiwa Pereira Ame Silima, aliyekuwa mbunge wa Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Injinia Masauni anaingia wakati zile tuhuma alizokumbwa nazo za kughushi umri, hazijachunguzwa ingawa ndizo zilizosababisha avuliwe uenyekiti wa UVCCM wakati wa kikao cha Baraza Kuu la UVCCM lililofanyika mjini Iringa mwaka 2010.

Uamuzi huo ulifanywa chini ya kilichoonekana kama njama za mapinduzi ya uongozi wa Injinia Masauni na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Mohamed H.N Moyo.

Makamu mwenyekiti Benno Malisa akiungwa mkono na kundi lenye nguvu la Ridhwan Kikwete, ambaye ni Mjumbe wa Baraza hilo, ndiye akateuliwa kushika wadhifa huo wa uenyekiti.

Siri ya tuhuma za kughushi dhidi ya Masauni ilitolewa kikaoni hapo na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Kikwete, aliyekuwa pia rais wa Jamhuri, aliposema “amejimaliza mwenyewe.”

Kikwete awali hakutaka kuzungumzia suala hilo, lakini baadaye aliwauliza wajumbe wa mkutano, “hivi mlielewa vizuri kilichomfanya Masauni ajiuzulu.”

Alijibiwa kwa sauti “hatujuiiiiii.” Ndipo aliposema, “Kilichomponza Masauni ni kutokuwa mkweli kuhusu umri wake. Alikuwa na tuhuma za kughushi umri uliomwezesha kushinda uchaguzi mwaka 2008.

“Tulipochunguza ilibainika ni kweli alighushi, alisema alizaliwa mwaka 1979, lakini ukweli alizaliwa mwaka 1973 na alianza darasa la kwanza mwaka 1979. Kwa hivyo hakuna aliyeonewa, aliyefitini na wala watu wasitafute mchawi katika hili. Hatua kama hii ilikwishafanyika kwa watu kama akina Nape.”

Nape Nnauye alinyimwa nafasi ya kugombea ilipobainika umri wake ulishapita kigezo cha kugombea nafasi aliyoomba katika UVCCM.

Kikwete alimfariji Masauni akimuita mkakamavu na mchapakazi, na akaahidi kumpangia kazi nyingine.

Uamuzi wa kuwashinikiza Masauni na Moyo kujiuzulu ulionekana na baadhi ya wajumbe, ni mpango wa kumpindua ili kuwekwa viongozi wanaomtii Ridhwan, katika hatua za kujipanga kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010.

Malisa aliteuliwa kukaimu nafasi hiyo na katika hotuba yake baadaye, alipongeza hatua Baraza kuwang’oa viongozi wenzake hao, kwa vile ni kitendo cha kishujaa na ishara ya jumuiya kukomaa.

error: Content is protected !!