Thursday , 30 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Magufuli ampongeza Waziri Aweso, amuonya ‘ningekufukuza’
Habari za Siasa

Magufuli ampongeza Waziri Aweso, amuonya ‘ningekufukuza’

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, John Pombe Magufuli, amemuagiza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kutowachekea wakandarasi wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Shinyanga…(endelea).

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo Ijumaa tarehe 29 Januari 2021, katika uzinduzi wa mradi wa maji wa Isaka-Kagongwa, wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga.

Sambamba na hilo, Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Maji kuwatumia wahandisi wazawa kama washauri katika miradi ya maji ili kuleta matokeo chanya.

“Usicheke na wakandarasi, cheka na maji wakati unayanywa, lakini kandarasi usicheke nao, na nikuombe katibu mkuu na naibu katibu mkuu wale ma-Consultant (washauri), mnaoweka kusimamia kwenye miradii hii. Ikiwezekana tafute wahandisi wenu wawe ‘local consultant’ kwa ajili ya kusimamia na kuleta matokeo chanya ya miradi hii,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amewaagiza Aweso na wahandisi wa wizara hiyo kuhakikisha miradi ya maji isiyokamilika, inakamilika mara moja.

“Nataka waziri (Aweso), miradi ambayo ilikuwa haijakamilika, wewe pamoja na watendaji wako walioko ndani ya wizara na wahandisi wote nchi nzima wanaoshughulika na maji, kila mmoja katika eneo lake wahakiksihe miradi iliyoko kwenye maeneo yenu inakamilika,” amesema Rais Magufuli.

Kiongozi huyo wa Tanzania amesema, katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake, Wizara ya Maji ilimsumbua kutokana na kushindwa kukamilisha miradi yake kwa wakati.

“Wizara ya maji ni katika wizara iliyonitesa miaka mitano iliyoita na hili nataka niseme, miradi ilikuwa haikamiliki, katika kipindi cha muda mrefu miradi iliyokuwa inakamilika haizidi asilimia 30 ya iliyoanzishwa. Na miradi mingi ilikuwa ya gharama kubwa yameweka humo mambo ambayo ni wizi,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo alipokuwa anazungumzia hatua ya Aweso ya kuwafukuza wakandarasi wawili (M.A Kharafi&Sons na Badr East Africa Enterprises), walioshindwa kukamilisha kwa wakati mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe.

“Nashukuru umeanza kuchukua hatua kwa wakandarasi feki kule Mwanga ya kuwafukuza, sababu ungechelewa kuwafukuza ningekufukuza wewe, ni vizuri uwe unawahi wale wanaokuchelewesha,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesisitiza “ Fukuza tu, sababu hawakuja huku kutangaza mambo ya michezo, wamekuja kufanya kazi. Ukitaka hela ya Tanzania lazima ufanye kazi.”

Kuhusu wakandarasi hao waliositishiwa mkataba wao Desemba 2020, Rais Magufuli ameagiza Bodi ya Wakandarasi Tanzania (CRB), kuwafutia usajili pamoja na kutowapa zabuni yoyote nchini.

“Kwa hiyo, uliowafukuza kwenye mradi, zungumza na bodi ya makandarasi kupitia Sheria namba 17 ya mwaka 1997, wafutwe wasipate kazi yoyote Tanzania nzima,” ameagiza Rais Magufuli.

Pia, Rais Magufuli amemuagiza Waziri Aweso kupeleka majina ya wakandarasi hao katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Na kwa vile pia tuna ushirikiano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, upeleke pia majina yao kule. Hatuhitaji makandarasi matapeli, tunataka mtu akipewa pesa za Watanzania masikini wakamilishe miradi,” amesema Rais Magufuli.

Wakandarasi hao walifukuzwa na Aweso mwishoni mwa mwaka 2020, kisha mradi huo unaogharimu Sh. 62 bilioni, umekabidhiwa kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa).

Kuhusu mradi huo wa maji aliouzindua, Rais Magufuli amesema utasaidia kutatua changamoto ya uhaba wa maji.

“Nimekuja hapa kuzindua mradi mkubwa wa maji wa Kagongwa na Isaka ambao umegharibu Sh. 23.157 bilioni ambazo zote zimetolewa na Serikali ya Tanzania. Kama mlivyosikia kabla ya ujenzi wa mradi huu miji hiyo ilikuwa na shida kubwa ya maji,” amesema Rais Magufuli.

“Mahitaji yalikuwa ni lita 4.6 milioni, Kagongwa lita 2.9 milioni, Isaka lita 1.6 milioni kwa siku. Upatikanaji wa maji ulikuwa lita 252,000 sawa na asilimia 6.3, Kagongwa walikuwa wanapata asilimia 3.6 na Isaka asilimia 9,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, mradi huo una uwezo wa kuzalisha lita 9,832,600 kwa siku ambao utahudumia watu 115,660.

“Mradi huu unauwezo wa kuzalisha maji lita 9,832,600 na hii ni kwa siku sawa na asilimia 203.33 ya mahitaji ya maji ya miji hii miwili, tukaamua mradi huu kuhudumia kwenye vijiji 22, unahudumia watu 115,660,” amesema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Aweso amesema mradi huo umegharimu Sh. 23.1 bilioni ambao unatoa maji kutoka Ziwa Victoria mkoani Mwanza hadi Kagongwa na Isaka mkoani Shinyanga huku akiahidi kutekeleza maagizo ya Rais Magufuli.

 

Baada ya kumaliza kuzindua mradi huo na kutoa maagizo, Aweso aliweka picha ya Rais Magufuli akizindua mradi huo kwenye akaunti yake ya facebook na kuandika “Mungu wetu ni mwema sana; Daima tumtangulize mbele.”

“Asante sana Mh. Rais kwa uzinduzi wa mradi wa Isaka-Kagongwa mkoani Shinyanga.
Tumepokea pongezi kwa wizara yetu kwa mioyo ya shukrani na tumeyapokea maelekezo, ushauri na maagizo yote kwa umakini na masikio yaliofunguka na mioyo ilio tayari kutekeleza,” ameandika Aweso ambaye pia ni Mbunge wa Pangani (CCM).

Amemalizia kuandika akisema “kwa wananchi na Watanzania wenzangu, niwaahidi hatutowaangusha na kwa uwezo wa aliye juu hii kazi tunaiweza.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

TEMESA iliyokarabati Kivuko kwa Bil 7.5 yapata hati chafu

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

ACT-Wazalendo yakusanya Mil 8.5/- kodi ya zuio na kutokomea nazo

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

DC Kasilda Mgeni ahamasisha chakula shuleni

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni...

Habari za Siasa

Bilioni 223.9 zapelekwa Tunduru ndani ya miaka 2 ya SSH

Spread the love  ZAIDI ya Sh. bilioni 223.9 zimepelekwa Wilaya ya Tunduru...

error: Content is protected !!