May 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli amlilia mbunge Nditiye

Rais John Magufuli

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge, Job Ndugai kufuatia kifo cha Mbunge wa Muhambwe (CCM), mkoani Kigoma, Mhandisi Atashasta Nditiye. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Nditiye alifikwa na mauti jana Ijumaa saa 4 asubuhi tarehe 12 Februari 2021, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, alipokuwa amelazwa kwa matibabu baada ya kupata ajali ya gari 10 Februari 2021, jijini humo.

Taarifa iliyotolewa na Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu ilisema, Rais Magufuli amemtaka Spika Ndugai kufikisha salamu zake za pole kwa familia ya marehemu, wabunge, wananchi wa jimbo la Muhambwe, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na kifo cha Mhandisi Nditiye.

Rais Magufuli amewataka wafiwa wote kuwa na moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi ya kuondokewa na mpendwa wao na amemuombea marehemu Nditiye apumzike mahali pema peponi, amina.

Nditiye aliyezaliwa tarehe 17 Oktoba 1969, amekuwa mbunge wa Muhambwe tangu mwaka 2015 hadi mauti yalipomfika jana Ijumaa.

Anakuwa mbunge wa pili wa Bunge hili la 12 kutoka Chama Cha mapinduzi (CCM), kufariki dunia, akitanguliwa na Martha Umbulla wa Viti Maalum, Mkoa wa Manyara aliyefariki tarehe 21 Januari 2021 nchini India alikokuwa amepelekwa kwa matibabu.

error: Content is protected !!