May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli alivunja Jiji la Dar, watumishi wake…

Rais John Magufuli

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, John Magufuli, ameivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kuipandisha hadhi Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaan … (endelea).

Rais Magufuli, amechukua uamuzi huo leo Jumatano tarehe 24 Februari 2021, kupitia taarifa kwa umma, iliyotolewa na Waziri, Ofisi ya Rais- Tamisemi, Selemani Jafo.

Waziri Jafo amesema, watumishi wa waliokuwa halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliyovunjwa, watapangiwa vituo vipya vya kazi.

Mapema leo asubuhi Jumatano, Rais Magufuli, akizindua Daraja la Juu la Kijazi, lililopo Ubungo, Dar es Salaam, alisema anakusudia kulivunja jiji hilo ili gharama zilizokuwa zinatumika kuendesha halmashauri hiyo zielekezwe kwenye miradi mingine.

“Nategemea kufanya mabadiliko kidogo, mabadiliko haya ya kuwa na manispaa ambazo zinawakilisha maeneo halafu unakuwa na jiji ambalo linakaa halina maeneo yoyote, natarajia Jiji la Dar es Salaam kulivunja, nawaambia hapa ili tutengeneze jiji la eneo fulani.”

“…lakini kuwa na madiwani wanakaa juu, wanachangiwa hela na hawana miradi ya maendeleo, wanakula posho na hawakuchaguliwa na watu. Hili nitalikataza. Wale wanaojiandaa kuwa mameya wa Dar es Salaam na wanakaa hawana maeneo, wajue hilo limekwisha,” alisema Rais Magufuli.

Amesema, Waziri Jafo, tayari amempa muswada wa sheria kwa ajili ya kufanya mabadiliko hayo ambayo yataruhusu manispaa moja yenye nguvu ndani ya jiji hilo kuwa jiji.

“Mjiandae kisaikolojia, wale waliokuwa wanataka Umeya wa jiji, Meya atapatikana Ilala au kutoka kwenye manispaa moja wapo hapa, na draft (muswada) nimeletewa na Jafo, nikitoka hapa nitakwenda kusaini,” amesema Rais Magufuli.

Alisema, fedha zilizokuwa zikitengwa kwa ajili ya kugharamia jiji hilo, zitapelekwa katika miradi ya maendeleo.

“Ukiwa na manispaa nne au tano, halafu unakuwa na madiwani hawawakilishi maeneo yoyote. Wanawakilisha manispaa zao halafu wanatengewa bajeti, hizo fedha ni vizuri zikapelekwa kwenye miradi ya barabara,” alisema Rais Magufuli.

error: Content is protected !!