January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli ala kiapo kuwa Rais wa Tanzania

Spread the love

RAIS wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungamo wa Tanzania, Dk. John Magufuli ameapishwa leo katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Shughuli ya kuapisha Rais Magufuli imefanywa na Jaji Mkuu Othman Chande, huku ikishihudiwa na Rais anayemaliza muda wake, Jakaya Kikwete, Rais wa Awamu ya tatu, Benjamini Mkapa, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na Spika wa Bunge, Anne Makinda.

Pia walikuwepo viongozi wa dini, mabalozi na viongozi mbalimbali waandamizi serikalini na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Sherehe hiyo pia imehudhuriwa na marais kutoka nchi mbalimbali za Afrika ikiwa ni pamoja na Rais wa Afrika Kusin, Jacob Zuma; Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila.

Mbali na marais hao pia walikuwepo Rais wa Rwanda, Paul Kagame; Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe na Rais Zambia, Edgar Lungu.

Hata hivyo, marais wa nchi nyingine za Afrika wametuma wawakilishi ambapo mataifa ya Ulaya na Marekani pia yamewakilishi na mabalozi wao hapa nchini.

Rais Magufuli ameapishwa, huku siku ya leo ikitangazwa jana na Rais Kikwete kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu kuwa ni mapumziko lengo likiwa ni kutoa nafasi kwa wananchi kushuhudia shughuli hiyo ya kumwapisha Rais wa Awamu ya Tano.

Baada ya Rais Magufuli kuapishwa, alipigiwa mizinga 21 na kisha kukagua gwaride.

Katika sherehe ya kuapishwa Rais Magufuli, vyama vya upunzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) vimesusia kushiriki kwenye shughuli hiyo.

Madai ya Ukawa ni pamoja na kwamba “uchaguzi mkuu haukuwa wa huru na haki” hivyo kukosa uhalali wa kumtoa Rais wa Awamu ya Tano.

Ukawa wamedai, kura za mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendele (Chadema) anayeungwa na Ukawa, Edward Lowassa ziliibwa na kuongezewa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Magufuli.

Akitangaza matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais wiki iliyopita Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu, Damian Lubuva alisema Rais Magufuli alichaguliwa kwa kura 8, 882, 935 sawa na asilimia 58.46 ambapo Lowassa alitangazwa kupata kura 6, 072, 848 sawa na asilimia 39.97 ya kura zote.

error: Content is protected !!