August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli ajiapiza ‘kuwamaliza’ Mdee, Bulaya

Wabunge Ester Bulaya na Halima Mdee

Spread the love

RAIS John Magufuli, amempongeza Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua anazochukua dhidi ya wabunge “wasumbufu” na kuahidi kuwashughulikia zaidi watakapokuwa nje ya Bunge, anaandika Charles Willliam.

Rais Magufuli ameyasema hayo, Ikulu jijini Dar es Salaam alipokuwa akipokea ripoti ya usafirishaji wa mchanga wa dhahabu – maknikia ambapo amedai kuwa wapo wabunge wanaotumia vibaya kinga yao na kwamba yeye atawachukulia hatua zaidi baada ya kufukuzwa bungeni.

“Mheshimiwa Spika endelea hivyo hivyo kule bungeni, wafukuze waropokaji wote ili wakose pa kuropokea na wakija kuropoka huku nje tutawashughulikia kwasababu wakiwa ndani ya bunge wanakuwa na kinga,” amesema na kuongeza;

“Wakishakuwa huku nje na wakaropoka mimi nakuahidi, I will deal with them (nitashughulika nao).”

Kauli ya Rais Magufuli ni kama msumari wa mwisho kwa wabunge Halima James Mdee wa Kawe na Ester Amos Bulaya wa Bunda Mjini – wote Chadema, ambao wamefungiwa kushiriki vikao vya Bunge mpaka mwakani kutokana na kudaiwa kudharau kiti cha Spika.

Adhabu hiyo kwa Mdee na Bulaya inafuatia mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Bunge ya Kinga, Haki na Maadili ambayo yalipata Baraka za wabunge walio wengi pamoja na kiti cha Spika.

Katiba ya Tanzania Ibara 101 inawalinda wabunge kutohojiwa wala kuchukuliwa hatua nje ya Bunge kutokana na kauli wanazozitoa ndani ya Bunge, kauli ya Rais kuwa atawashughulikia wabunge wanaofukuzwa bungeni inalenga kuwapa wakati mgumu Mdee na Bulaya.

Tayari wabunge hao wametangaza kuliburuza mahakamani Bunge, wakipinga kufukuzwa pasipo kuhojiwa wala kusikilizwa. Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema amethibitisha kuwa hatua za kulifikisha mahakamani Bunge zinaendelea.

error: Content is protected !!