Wednesday , 8 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Magufuli aizungumzia Chato
Habari za SiasaTangulizi

Magufuli aizungumzia Chato

Julius Nyerere, Hayati Baba wa Taifa
Spread the love

RAIS wa Tanzania, John Magufuli amesema Wilaya ya Chato iliyoko mkoani Geita, ilianza kujengwa na Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Kiongozi huyo wa Tanzania amesema hayo leo Jumatatu tarehe 11 Januari 2021 wakati anaelezea historia ya wilaya hiyo, katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda Chato mkoani Geita.

Hafla hiyo iliyohudhuriwa na Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi ambapo, Rais Magufuli amesema baada ya Mwalimu Nyerere kuondoka madarakani, marais waliofuata walifika wilayani humo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.

“Kwa hiyo wewe Rais Nyusi umefika hapa palipo buniwa na kuanzishwa na Mwalimu Nyerere, baada ya Nyerere kuondoka marais wengine waliofuata, walifuata kuja hapa,” amesema Rais Magufuli.

Rais John Magufuli

Rais Magufuli amesema, Chato imetembelewa na Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, Hayati Benjamin Mkapa (Rais awamu ya tatu), ambaye alikitangaza Kijiji cha Chato kuwa wilaya na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete aliyezindua rasmi kuwa wilaya.

“Alikuja Rais Mwinyi alifika hapa, baada ya Mwinyi kuondoka, alikuja tena Mzee Mkapa, akakitangaza Kijiji cha Chato kuwa wilaya, baada ya Mkapa kuondoka alikuja Mzee Kikwete akazindua rasmi Wilaya ya Chato,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amesema “Na wewe sasa (Rais Nyusi) umekuja hapa kuweka jiwe la msingi la Hospitali ya Kanda itakayohudumia watu takribani milioni 18.”

Amesema, siku Mwalimu Nyerere anafungua kiwanda hicho, yeye alikuwa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Chato.

Marais wastaafu wa Tanzania

Akielezea zaidi historia ya Chato, Rais Magufuli amesema dhana ya Tanzania kujitegemea kiuchumi, iliasisiwa na Mwalimu Nyerere wilayani humo.

Rais Magufuli amesema, Mwalimu Nyerere aliasisi dhana hiyo tarehe 9 Januari 1967, alipokwenda kufungua Kiwanda cha Pamba cha Chato wilayani humo.

“Historia ya Chato ni ndefu, mwaka 1967 aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Nyerere alifika Chato, wakati huo ilikuwa bado kijiji cha Chato, akaja akafungua Kiwanda cha Pamba cha Chato kilichojengwa kwa thamani ya Sh.2 milioni kwa wakati huo,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, wakati anafungua kiwanda hicho, Mwalimu Nyerere aliitisha harambee ya wananchi kuchangia ujenzi wa Bandari ya Nyamirembe, ambayo hadi sasa inafanya kazi.

“Na siku ya ufunguzi Mwalimu Nyerere, alinzisha mchango wa wananchi waliokuwepo pale, katika kujenga dhana ya kujitegemea na yeye akachangia katika mchango huo Paundi 1,000 ilikuwa sawa na Sh.2,000,” amesema Rais Magufuli ambaye ni mzaliwa wa Chato.

Rais Magufuli amesema “Akachangia siku hiyo na wengine, kwa ajili ya kuanza kujenga bandari ya Nyamirembe. Hiyo ndio ilikuwa dhana ya Mwalimu Nyerere katika kijiji cha Chato.”

Kiongozi huyo wa Tanzania amesema, baada ya Mwalimu Nyerere kuitisha harambee hiyo, tarehe 5 Februari 1967 alikwenda mkoani Arusha na kutangaza Azimio la Arusha.

“Wiki mbili baadae, alienda Arusha akatangaza Azimio la Arusha, dhana ya kujitegemea aliianzisha hapa kwa kuchangia 2,000 kwa ajili ya kujenga Bandari ya Nyamirembe na ipo bado inafanya kazi,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, Kiwanda cha Pamba cha Chato kilijengwa na Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kutengeneza na kusafirisha marobota 20,000 ya pamba kwa mwaka.

Akielezea ziara ya Rais Nyusi nchini Tanzania, Rais Magufuli amesema ziara hiyo imelenga kuendeleza na kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili, hususan wa kibiashara na undugu.

“Rais Nyusi anayajua maisha ya Watanzania, kwa hiyo ni rafiki wa Tanzania. Lakini urafiki wa Tanzania na Msumbiji ni wa muda mrefu. Tangu Mwalimu Nyerere pamoja na Mwalimu Samora Machel ambaye alikuwa mwanzilishi wa Msumbiji, sisi ni ndugu,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Msumbiji unazidi kuimarika.

“Ndani ya Serikali tuna makubaliano ya kufanya kazi pamoja kwa kushirikiana, biashara ya sasa hivi kati ya Tanzania na Msumbiji imeongezeka. Mwaka jana ilifikia Sh.93.6 bilioni, kuna makampuni ya Msumbiji yanafanya kazi hapa, na kuna makampuni ya Tanzania yanafanya kazi Msumbiji,” amesema Rais Magufuli.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Bunge labaini madudu mfumo ukusanyaji mapato, h’shauri tatu kikaangoni

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali...

Habari za Siasa

Mkuu wa wilaya ya Rungwe azindua vyumba sita vya madarasa vya thamani ya 64 mil

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu amezindua vyumba...

Habari za Siasa

Mbunge afurahia mabilioni ya Samia kutua jimboni

Spread the love  MBUNGE wa Igunga, Nicholas Ngassa ameishukuru Serikali kwa utekelezaji...

Habari za Siasa

PIC yaishauri Serikali kuanzisha mfuko wa uwekezaji kusaidia mashirika ya umma

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji...

error: Content is protected !!