May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli aisimamisha Mwanza, mwili wazungushwa mara 5 uwanjani

Spread the love

 

MWILI wa Dk. John Pombe Magufuli, aliyekuwa Rais wa Tanzania, umezungushwa mara tano, ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Maelfu ya wakazi wa Mwanza na maeneo jirani, wamejitokeza kwa wingi na kuujaza uwanja huo, leo Jumatano tarehe 24 Machi 2021, wakiongozwa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Majaliwa amesema, kujitokeza kwa wingi kwa wananchi kumuaga Dk. Magufuli ni ishara kwamba alikubalika na “ameacha alama taifa zima, ndio maana kila sehemu wanalia kutokana na utumishi wetu.”

Mzunguko huo wa mwili wa Dk. Magufuli, umeanza saa 5:03 asubuhi ambapo waombolezaji waliokuwapo uwanjani hapo, walipata fursa ya kumuaga mpendwa wao na ulihitimisha saa 5:15 asubuhi.

Mara baada ya kumaliza mzunguko huo, mwili wa Dk. Magufuli aliyefariki Jumatano ya tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam, ulianza kuzungushwa mitaa mbalimbali ya Jiji la Mwanza.

Mzunguko kama huo wa mara tano, ulifanyika Jumapili ya tarehe 21 Machi 2021, katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, kwa waombolezaji waliojitokeza kumuaga kiongozi wao.

Baada ya kumaliza mzunguko wa jiji Mwanza, mwili wa Dk. Magufuli utasafirishwa kwenda nyumbani kwao Chato ambako kesho Alhamisi utaagwa na Ijumaa utazikwa.

Katika maeneo yote ya Mwanza ulipopita msafara huo, watu walikuwa wengi sana na kusimamisha shughuli mbalimbali za wananchi, ili kuwawezesha kumuaga mpendwa wao.

Msafara wa kwenda Chato kwa barabara utapita Busisi- Sengerema- Geita- Buseresere- Katoro- Bwanga na kisha Chato.

Hii mara tano inaweza kuwa historia kwa Dk. Magufuli ikiwa na maana kuwa; aliingia madarakani kwa mara ya kwanza tarehe 5 Novemba 2015, alikuwa Rais wa awamu ya tano, ameongoza kwa miaka mitano na amefariki Jumatano.

error: Content is protected !!