MGOMBEA urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pombe Magufuli ameeleza kuhofia jazba katika upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 20202. Anaripoti Mwandishi Wetu, Bukoba … (endelea).
Akihutubia wananchi wa Kemondo-Bukoba Vijijini na Watanzania jana Jumanne tarehe 15 Septemba 2020 aliwaomba kumchagua ili aendelee kuiongoza Tanzania kwa miaka mitano mingine.
“Tusichague kwa jazba na kuangalia viongozi wapenda maneno, tukikosea tutajuta maana hakuna maendeleo mtakayoyaona,” amesema Dk. Magufuli.
Alisema, ingawa urais ni mateso, anaomba Watanzania wamruhusu kumaliza kipindi chake cha pili kisha apumzike.
Kauli ya kutoongeza dakika hata moja baada ya miaka mitano ijayo ya utawala wake, alikuwa akiirudia mara kwa mara.
“Naombeni mnipe miaka mitano tu, tutafanya makubwa katika muda huo, nikimaliza miaka yangu mitano hiyo, sitaki niongezewe hata siku moja, wapo wengine ndani ya CCM wanaoweza pia kuongoza, nataka nipumzike na mimi niangalie wengine wanavyofanya kazi,” alisema
“Sio kwamba napenda niwe rais, urais ni mateso, kazi yoyote ukitaka kuifanya vizuri ni mateso, nasema kwa dhati nikishamaliza miaka hii mitano sitaki kuongezewa hata siku moja.”
Akizungumzia mafanikio ndani ya miaka mitano ya utawala wake iliyopita, alisema Muleba imenufaika na zaidi ya Sh.65.32 bilioni zilizotolewa kwenye miradi ikiwemo ya afya, elimu, miundombinu na mingine.
Leave a comment