January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli agonga mwamba Z’bar

Spread the love

LICHA ya kauli za vitisho zilizotolewa na Rais John Magufuli wakati akizungumza na wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) jijini Dar es Salaam wiki iliyopita kwamba, atawashughulikia watakaoleta fyokofyoko, Wazanzibari wamepuuza, anaandika Faki Sosi.

Kassim Bakar Ali, Mwenyekiti wa Jahazi Asilia ambaye pia alikuwa mgombea urais Zanzibar kwenye uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana amesema, Zanzibar ina historia ya migogoro ya kisiasa.

Amesema, imekuwa kwenye migogoro ya uchaguzi tangu mwaka 1957 na kwamba, jeshi halikuweza kuiondoa hivyo kuamini nguvu ama kutumia jeshi ndio muafaka ni kuchemsha.

Kassim ameonya kwamba, kutumia jeshi kutachangia kuchochea mgogoro wa kisiasa na hata kusababisha machafuko visiwani humo.

Amesema yeye na chama chake hawana imani na jeshi hilo kwa kuwa nao hushiriki katika kuiba kura “hatunaimani na jeshi kutokana na kuwa wao ni wasisimamizi wa wizi wa kura.”

Faki Rashid Maalim Mkazi wa Bububu, Unguja amesema, kilichofanywa na Rais Magufuli ni kuwatia hofu Wazanzibari na wao wametambua hilo.

“Alitumia maneno yale kutia hofu tu, lakini hakuna asiyejua kwamba CCM wanaitaka Zanzibar kwa gharama yoyote lakini pia naamini kwamba, haki hutafutwa na Wazanzibari wakiamini hilo hawatakuwa na hofu,” amesema na kuongeza;

“Tunajua ni vitisho tua, hata alipoanza kwa kutaja sijui Dodoma, Nachingwea, Ukerewe lakini mwisho wa kauli alifikia kwenye kiini chake na kuitaja Pemba na Zanzibar kwa maana ya Unguja kuwa ndio kuna mateso ya kisiasa.”

Hata hivyo, Abdallah Kombo Khamis, aliyekuwa mgombea wa urais kupitia Chama Democratic Part (DP) amesema, kauli ya Rais Magufuli kwamba hausiki na suala la Zanzibar huku yeye akiwa Amiri Jeshi Mkuu ni kukimbia majukumu.

“Yeye ni Amiri Jeshi wa Tanzania au wa CCM? kwani amekuwa akikitumikia chama chake bila kujali maslahi ya wananchi wake,” amehoji Kombo.

Amesema kuwa, wananchi wa Zanzibar tayari wamezoea kuonewa na kupigwa kama walivyofanyiwa miaka iliyopita.

“Mimi mwenyewe ni muhanga wa machachuko na vurugu zilizowahi kutokea miaka iliyopita kwani nilipoteza kaka yangu kwa kupigwa risasi na askari na mjomba wangu kupigwa risasi ya mguu mpaka leo ni mlemavu,” amesema Kombo.

Seif Ali Iddi aliyekuwa mgombea kupita chama NRA amesema kuwa, Wazanzibari wapo njiapanda kutokana na Rais Magufuli kukwepa kutatua mgogoro wa kisiasa visiwani humo.

Amesema kuwa, Rais Magufuli anakwepa kuhusika kutokana na kuwa chama kilichomuweka madarakani ndicho kinachoshika sukani wa dhuruma visiwani humo huku akibainisha kuwa, mgogoro wa kisiasa viswani humo ni wa kihistoria.

error: Content is protected !!