Tuesday , 5 December 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Magufuli aeleza walivyochambua, kujadili wagombea ubunge
Habari za SiasaTangulizi

Magufuli aeleza walivyochambua, kujadili wagombea ubunge

Rais John Magufuli, Mwenyekiti wa CCM
Spread the love

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Rais John Pombe Magufuli, imewataka wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, kumtanguliza Mungu na kuweka mbele maslahi ya chama na Taifa wakati wakijadili na kuteua wagombea ubunge wa chama  hicho. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Rais Magufuli ametoa nasaha hizo leo Alhamisi tarehe 20 Agosti 2020 wakati akifungua kikao cha Halmashauri Kuu kinachofanyikia Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma.

Kikao hicho, kinakazi ya kuteua wagombea ubunge wa majimbo na viti maalum watakaoshiriki katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020.

Amesema, mchakato wa uteuzi ndani ya chama hicho ulianza takribani mwezi na nusu uliopita ambapo wajumbe walipiga kura za maoni na kupendekeza majina ya wagombea kisha kujadiliwa kwenye vikao vya ngazi mbalimbali na sasa wamefika kwenye kikao hicho ili wajadiliwe.

Rais Magufuli amewapongeza wagombea wote wa Chama Cha Mapinduzi waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali kwani walijitokeza wanachama wengi sana na hii ilitokana na kwamba chama wanakipenda.

“Wana CCM 10,367 walichukua fomu nafasi ya jimbo na viti maalum. Wana CCM waliojitokeza kuwania ubunge katika  baraza la wawakilishi walikuwa 786.  Waliojitokeza kuwania udiwani, wadi na viti maalum walikuwa 33,094, kwa maana hiyo, waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali ndani ya CCM walifika 43,461,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, makundi mbalimbali yaliomba nafasi hizo wikiwemo vijana, wakulima, wafanyakazi, wavuvi, watu wenye ulemavu na viongozi wa taasisi zisizo za kiserikali pamoja na wanawake.

Amesema, “uchambuzi ulikuwa wa kina kwelikweli, tulitumia taarifa nyingi kutoka kwenye vyanzo mbalimblai na mimi nataka kuwahakikishia ndugu wajumbe nimesoma majina yote 10,367.”

Rais Magufuli amesema, chama hicho kimekusanya taarifa za kila mgombea na kwamba  ufafanuzi juu yao upo wazi, “yule anayetaka ufafanuzi wa mtu yoyote, lakini kamati kuu tulikaa na kuchambua ili kurahisisha kazi ambayo mtaifanya leo hii.”

“Ilitubidi tufanye uchambuzi wa kina kwa sababu ya unyeti wa nafasi wanazogombea, ilikuwa lazima tujiridhishe wagombea wawe watu wenye uwezo wa kupeperusha bendera ya chama chetu na hatimaye kukipa ushindi chama chetu,” amesema.

“Kama mnavyofahamu, miongoni mwa wabunge na wawakilishi, ndio atakapopatika waziri mkuu na miongoni mwa hao atapatika makamu wa pili wa urais Zanzibar, Spika, manaibu na wenyeviti, pia watapatikana mawaziri na naibu mawaziri, hivyo imetulazimu tutakaowachagua wawe na sifa ya kuwa viongizi,” amesema.

Rais Magufuli ambaye ni mgombea urais amewahakikishia wajumbe wa kikao hicho kuwa Kamati ya usalama imefanya kazi kubwa pamoja na kamati kuu ili kuwarahisishia wajumbe hao kuteua.

“Ndugu wajumbe, nawasihi muweke maslahi ya taifa mbele, msichague kwa urafiki, undugu, ukanda au ukabila, tangulizeniu mbele maslahi ya taifa,” amesema.

Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally alisema, kwa mujibu wa katiba ya chama, kikao hicho ndicho kinachotakiwa kufanya uteuzi wa wagombea kwa nafasi ya ubunge na uwakilishi.

“Lakini kutokana na ratiba za tume zetu za uchaguzi za NEC na ZEC kupishana, kikao hiki hakitafanya nafasi za uwakilishi, kitafanya ubunge wa majimbo na viti maalum,” amesema Dk. Bashiru.

Kuhusu akidi, Dk. Bashiru amesema idadi ya wajumbe wa kikao ni 167, “lakini wajumbe 54 hawawezi kushiriki kikao hiki kwani wamegombea ubunge na uwakilishji. 42 wamegombea ubunge na 12 uwakilishi, hawa nao watajadiliwa humu humu.”

Alisema waliohudhuria kikao ni 113 ambao ni zaidi ya nusu ya wajumbe huku wajumbe wawili wakiwa ni wagonjwa.

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM

Kabla ya kuanza kwa kikao, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey  Polepole alisema, “kikao cha leo kwa asili ya majukumu yake ni kikao cha ndani, tutakuwa na waandishi wa habari hadi pale mwenyekiti atakapoingia, atafungua mkutano na baada ya kufungua, tutaomba mtupishe.”

Polepole alisema, baada ya kikao kumnalizika, atazungumza na waandishi wa habari kutoa taarifa ya kile kilichojili.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online, MwanaHALISI TV na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Baba yake Ole Sabaya ashinda Uenyekiti CCM – Arusha

Spread the loveLoy Thomas Sabaya ambaye ni Baba wa aliyekuwa Mkuu wa...

Habari za Siasa

Serikali yaagiza uchunguzi chanzo maporomoko Hanang

Spread the loveSERIKALI imeagiza uchunguzi ufanyike ili kubaini chanzo cha maporomoko ya...

Habari za SiasaTangulizi

Maafa Manyara: Rais Samia akatisha ziara yake Dubai

Spread the loveRAIS wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amekatisha ziara yake...

Habari za SiasaTangulizi

Wataalaam wa miamba watua Hanang

Spread the loveWaziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na...

error: Content is protected !!