November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli aagiza mishahara ‘watumishi’ TMAA ipunguzwe

Rais John Magufuli

Spread the love

RAIS wa Tanzania, John Magufuli ameagiza waliokuwa watumishi wa Wakala wa Ukauzi wa Madini Tanzania (TMAA) kisha kuhamishiwa Tume ya Madini wapunguziwe mishahara yao. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Kiongozi huyo wa Tanzania, ametoa agizo hilo leo Ijumaa tarehe 11 Desemba 2020, wakati anamuapisha Profesa Shukrani Manya, kuwa Naibu Waziri wa Madini, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Watumishi hao walihamishiwa Tume ya Madini Tanzania baada ya TMAA kuvunjwa rasmi Julai 2017, kutokana na sakata la makontena ya mchanga wa dhahabu zaidi ya 200 yaliyozuiliwa katika Bandari ya Dar es Salaam.

Mkaontena hayo, yalizuiliwa bandarini hapo kwa ajili ya kupisha uchunguzi kutokana na udanganyifu juu ya kiwango cha madini yaliyokuwamo ndani yake.

Rais Magufuli amesema, watumishi hao wanapaswa kupunguziwa mishara yao kwa kuwa walifanya kazi ya ovyo walipokuwa watumishi wa TMAA.

“TMAA mlipokuwa kule mlikuwa na mishahara mizuri na kile kitengo tulifuta sababu ya kazi mbaya, mlihamishwa kule, mlikuja na mishara yenu. Hiyo mishahara katibu mkuu kiongozi mpunguze, wale walitakiwa wawe wamepunguzwa sababu kazi waliyoifanya TMAA ilikuwa ya ovyo,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amemuagiza Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi kwa kushirikiana na Katibu Mkuu wa Utumishi washughulikie suala hilo.

Kiongozi huyo wa Tanzania amesema, kama kuna mtumishi asiyekubali kupunguziwa mshahara wake, ana hiari ya kuacha kazi.
“Hawa waliokuja ambao hawakufanya kazi vizuri wanateremshwa ili kama kuna ambao hawataki kutemreshwa waache kazi, wakatafute kazi nyingine, hii ndio meseji yangu,” amesema

“Katibu mkuu kiongozi ilitakiwa hili uwe umefanya mapema, kwa hiyo kampe maagizo katibu mkuu utumishi waanze kushushwa mshara,” ameagiza Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli ameagiza wanaolipwa mishahara zaidi ya Sh.15 milioni kwa mwezi wapunguziwe mishahara yao, huku akieleza mamlaka husika kuwaongeza mishahara watumishi wanaofanya kazi vizuri.

“Na hili halijaanzia kwa hao, wako wakurugenzi waliojipangia mishahara hadi milioni 25, nikasema mtu yeyote mishahara isiwe zaidi ya milioni 15,” amesema Rais Magufuli.

“Haiwezekani ukapelekwa tume ya madini ulikotoka kule na mshahara Sh. 10 milioni, ukamzidi mkurugenzi wako wakati wewe si mkurugenzi, yuko pale bosi wako anapokea milioni tano, wewe una milioni 10, hatuwezi kufanya hivyo, anayetakiwa kuzidiwa mshahara ni mimi, mimi napata milioni tisa, lakini mtu wa TRA (Mamlaka ya Mapato) ana milioni 15 na kadhalika,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema “naamini mmenielewa, napenda wanaofanya kazi vizuri wapate mishahara mizuri, wanaofanya vibaya nataka wakose kabisa au wapate kidogo sana ili iwe fundisho kwao. Wafanyaa kazi hawa TMAA walipata hela mno, najua huu ujumbe umeeleweka na wengine mliokuwa TMAA mishahara inapungua, mkishindwa acheni kazi.”

error: Content is protected !!