May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magufuli aagiza madaktari waliokimbia kazini watafutwe

Rais John Magufuli, akizindua ujenzi wa jengo la Idara ya Wagonjwa wa Huduma ya Dharura katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tabora

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, John Magufuli ameagiza madaktari wanaopangiwa ajira katika hospitali za umma kisha wanakimbilia kwenye hospitali binafsi kwa kigezo cha masilahi madogo, wachukuliwe hatua. Anaripoti Mwandishi Wetu, Tabora … (endelea).

Kiongozi huyo wa Tanzania ametoa agizo hilo leo Jumamosi tarehe 30 Januari 2021, wakati anaweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la magonjwa ya dharura ya Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Tabora.

Agizo hilo amelitoa baada ya kupewa taarifa za madaktari watatu wa hospitali hiyo, waliokimbilia katika hospitali binafsi kwa sababu ya mishahara midogo.
Taarifa hizo alipewa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Mark Waziri.

Rais Magufuli ameshauri madaktari hao wafungiwe kufanya kazi pamoja na hospitali wanazokwenda kutibia.

“Mfatilieni huyo daktari aliyekimbia na hiyo hospitali, ikiwezakana tuna mfungia dakatari, tunafungia na hospitali aliyoenda kutibia, ili watu wajifunze wizara ya afya sio ya kuchezea,” ameagiza Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, madaktari hao hawakupaswa kukimbia kwa kuwa walisomeshwa kwa fedha za Serikali.

“Unamsomesha mtu kwa fedha za masikini, wanachangia kusomesha madaktari na wanapata mkopo wa asilimia 100. Unamaliza pale unapelekwa hospitali, ukipelekwa kule unakimbia unasema masilahi madogo, hela yetu umekula halafu unasema masilahi madogo,” amesema Rais Magufuli.

Ameagiza Wizara ya Afya iwatafute madaktari hao waliokimbia, ili waeleze hela za Serikali zilizowasomesha ziko wapi.

“Na walisomemshwa na Serikali na hawajarudisha hizo fedha, watafute hao watu ili tuje tujue hela zetu ziko wapi. Sababu hakuna anayeridhika na msharaha, hata mimi siridhiki nao, hata manesi hawaridhiki lakini wanajituma,” ameagiza Rais Magufuli.

Rais Magufuli amewashauri madaktari wanaoajiriwa wasizibe nafasi za madaktari wengine, kwa kuomba ajira na kupewa kisha kuondoka katika vituo vyao vya kazi.

“Kwa nini aliomba kazi Serikalini akaziba nafasi za madaktari wengine kwa sababu kazi ya udaktari pia ni ya kujitoea kama sadaka. Hakuna mtu anayeridhika na mshahara.”

“Lakini kama alipewa kazi yake akaajiriwa na akanusa hapa, akaondoka pamoja na mshahara wetu kwa nini asishtakiwe kwa wizi” amehoji Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima amesema atalifanyia kazi agizo la Rais Magufuli la kuwatafuta madaktari waliohama katika hospitali hiyo.

Pamoja na agizo lake la kuongeza madaktari bingwa kwenye Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Tabora.

“Pamoja na maelekezo yako uliyotoa tutayafanyia kazi kuongeza madaktari bingwa na kuwafuatilia wale waliondoka, kwa nini wameondoka, tutafanyia kazi na tuko tayari kupokea maelekzo yako mengine,” amesema Dk. Gwajima.

Awali, Dk. Waziri alimueleza Rais Magufuli kwamba Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Tabora, inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa madaktari.

Dk. Waziri alisema miongoni mwa sababu za changamoto hiyo, madaktari wanaopangiwa hospitalini hapo kukimbilia katika hospitali binafsi kwa sababu ya masilahi madogo.

Mganga huyo mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Tabora, amesema alijaribu kuongea nao kuhusu mishahara yao bila mafanikio.

“Changamoto ambazo madaktari nilioongea nao wengi wanasema mshahara mdogo, anatoka Serikalini anaenda private,” amesema Dk. Waziri.

error: Content is protected !!