December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magoli 14 yafungwa ligi kuu, KMC yaongoza

Spread the love

MICHEZO ya raundi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2020/21 imemalizika huku ikishuhudia magoli 14 yakifungwa katika mechi kumi. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam…(endelea)

Pazia la ligi hiyo inayoshirikisha timu 18 lilizinduliwa Jumapili tarehe 6 Septemba 2020 kwa michezo sita na michezo miwili ikihitimishwa jana Jumatatu.

KMC FC ya Kinondoni Dar es Salaam, imeanza kwa kishindo ligi hiyo kwa ushindi wa 4-0 dhidi ya Mbeya City, mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Kati ya michezo hiyo tisa ya mzunguko wa kwanza ni timu saba ziliibuka na ushindi na michezo miwili ilienda sare.

Yanga imeanza kwa sare ya 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo uliochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Suluhu nyingine ilishuhudiwa katika mchezo uliopigwa CCM Gairo Mkoa wa Morogoro kati ya Mtibwa iliyowaalika Ruvu Shooting.

Wegeni wa ligi hiyo, Dodoma FC imeanza vyema ligi hiyo kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Mwadui katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Gwambina ya Mwanza na Ihefu ya Mbeya zimekaribishwa katika ligi hiyo kwa vipigo.

Biashara United ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Karume Mkoa wa Mara iliifunga Gwambina goli 1-0.

Bingwa mtetezi wa ligi hiyo, Simba yenyewe ilianza safari ya kutetea kombe hilo kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Ihefu kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Bringimana Blaise, mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi anayekipiga Namungo FC ya Lindi goli lake lilikuwa la kwanza kufungwa katika msimu wa ligi hiyo ya 2020/21.

Goli hilo pekee alilifunga katika Uwanja wao wa nyumbani wa Majaliwa dhidi ya Wagosi wa Kaya, Coastal Unioni na kuiwezesha kuibuka na ushindi wa 1-0.

Ligi hiyo itaendelea kwa mzunguko wa pili kuanzia Ijumaa tarehe 11 Septemba 2020.

error: Content is protected !!