August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Magazeti, Majarida 473 yafutwa

Magazeti yakiwa mezani yanauzwa

Spread the love

NAPE Nnauye, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo amefuta viapo vya usajili wa magazeti na majarida 473 kutokana na kutofuata sheria za magazeti, huku akitoa onyo kwa waliosajili masafa ya redio (Frequency) pasipo kuyafanyia kazi kwa muda mrefu, anaandika Regina Mkonde.

Nape ametoa taarifa hiyo leo katika mkutano na waandishi uliofanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dar es Salaam.

Nape amesema kuwa, uamuzi wa kufuta usajili wa magazeti na majarida hayo ni kutokana na wamiliki wake kutoyachapisha kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo hivyo kukiuka sheria za magazeti nchini.

“Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Msajili wa Magazeti iliyo chini ya Idara ya Habari (MAELEZO) Tanzania ina magazeti na majarida 881 yaliyosajiliwa kisheria.

“Licha ya magazeti na majarida kusajiliwa, yapo baadhi yameshindwa kuchapishwa na wamiliki mara baada ya kusajiliwa na mengine yalichapishwa kwa muda mfupi na kuacha kabisa uchapishaji,” amesema.

Amesema, magazeti yote nchini husajiliwa kwa mujibu wa sheria ya magazeti ya mwaka 1976 sehemu ya pili na kwamba, kwa mujibu wa kifungu cha 23 (1), waziri amepewa mamlaka ya kufuta hati za viapo zozote zilizoandikishwa na gazeti ambalo halikutolewa kwa muda wa miaka mitatu mfululizo baada ya kutangaza kusudio la kuyafuta magazeti husika kwenye gazeti la serikali.

“Wizara imefanya mapitio ya viapo vya usajili wa magazeti yote na ofisi ya waziri mwenye dhamana ya habari, imejiridhisha kuwa kuna idadi ya magazeti 473 ambayo yamesajiliwa lakini hayajachapishwa kwa zaidi ya miaka mitatu,” amesema na kuongeza;

“Kutokana na kufutwa kwa viapo vya usajiri wa magazeti hayo, mtu yeyote atakayechapisha au kusambaza magazeti yaliyotajwa katika tangazo hilo kwa njia ya nakala ngumu au kielekroniki atakuwa anakiuka sheria ya magazeti sura ya 229 kifungu cha 6 na hivyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.”

Amesema, iwapo kuna mmiliki wa gazeti ambaye angependa kuendelea na biashara hiyo baada ya kufungiwa, wanaruhusiwa kuwasilisha maombi mapya ya usajili kwa kufuata taratibu zilizopo.

“Iwapo kuna mmiliki ambaye angependa kuendelea na biashara hii baada ya kufungiwa, milango iko wazi kwa ajili ya kuwasilisha maombi mapya ya usajili kwa kufuata taratibu zilizopo. Ni imani yangu kuwa kwa wale wenye nia njema wameyaelewa maelezo haya,” amesema.

error: Content is protected !!