HALI ya taharuki, wasiwasi na hofu imetanda kwa saa kadhaa katika mji wa Christchurch nchini New Zealand baada ya watu kadhaa kufanya shambulizi kubwa kwenye misikiti miwili na kuuawa watu 49 huku 48 wakijeruhiwa. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa…(endelea).
Tukio hilo limetokea leo tarehe 15 Machi 2019 afajiri baada ya waumini wa Dini ya Kiislam kuhudhuria ibada ya alfajir kwenye msikiti wa Al Noor na Lin Wood iliyofikwa na mkasa huo.
Jacinda Arden, Waziri Mkuu wa New Zealand amezungumza na wanahabari katika mji mkuu wa nchi hiyo Wellington ambapo amesema, watu 10 waliofariki walishambuliwa katika msikiti wa kwanza wa Lin wood na 30 na baadaye watu tisa walipoteza maisha katika shambulio lililotekelezwa kwenye msikiti wa pili wa Al Noor.
Amesema, tukio hilo la kigaidi lilipangwa vilivyo na watuhumiwa kabla ya kutekelezwa akieleza kwamba, katika magari ya watuhumiwa kulikuwa na vifaa vya milipuko.
Arden amesema, tukio hilo linaashiria kwamba vitishio vya kiusalama katika taifa hilo vimeongezeka kutoka hali ya chini na kufikia kiwango cha juu.
Amewataka raia wa nchi hiyo kusikiliza ushauri wa polisi wa kwamba hali ya usalama iko vizuri.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa, Jeshi la Polisi limewaweka kizuizini wanaume watatu na mwanamke mmoja wanaotuhumiwa kuhusika katika tukio hilo la kigaidi ambapo majeruhi wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Christchurch.
Scott Morrison, Waziri Mkuu wa Australia ameeleza kusikitishwa na hatua ya raia wa nchi yake kujihusisha na vitendo vya kigaidi jambo ambalo linachafua taswiraya nchi hiyo.
“Australia na New Zealand sio washirika tu, sisi ni wa familia moja. Leo tunahuzunika, tumeshtuka, tunashangaa na tumekasirishwa na tukio hilo,” amesema Morrison.
Baada ya kutokea tukio hilo Serikali ya Washngton imeeleza kuchukua tahadhari zaidi kulinda raia wake wa dini zote.
Polisi wa Los Angeles, New York na Minneapolis wameeleza kuwa wataimarisha zaidi ulinzi katika miji yote baada ya kutokea shambulizi nchini New Zealand.
“Hakuna tishio lolote kwa sasa hapa Marekani kwenye misikiti lakini tutaongeza ulinzi zaidi,” imeeleza taarifa ya polisi wa Minneapolis.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa, washambuliaji waliandika kurasa 87 na kuziweka kwenye mitandao ya kijamii wakieleza namna wanavyokerwa na wahamiaji wa Dini ya Kiislam nchini New Zealand.
Leave a comment