Spread the love

 

SERIKALI kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea na majadiliano ya urejeshwaji wa mafuvu ya machifu yaliyochukuliwa na wakoloni hususani wajerumani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro … (endelea).

Hayo yamebainishwa na Rais Samia Samia Suluhu Hassan leo Jumamosi tarehe 22 Januari, 2022 katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika (MoCU) wakati akizindua Tamasha la utamaduni mkoa Kilimanjaro, ambalo pia alikuwa mgeni rasmi.

Rais Samia ametoa kauli hiyo baada ya Mwenyekiti wa Machifu nchini na Chifu mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Frank Mareale katika risala yake kumuomba Rais Samia kuyarejesha nchini mafuvu ya machifu ili yatumike kuelimisha jamii na shughuli za kitalii.

Katika risala yake Chifu Mareale pia alimuomba kuanzishwa kwa kazi data sahihi inayohusu machifu nchini, kuweka taarifa sahihi za machifu na mchango wao katika kupambana na ukoloni pia alimuomba kuhakikisha mapango yaliyotumiwa na machifu yatambuliwe na yatumike kwa shughuli za kitalii.

Pia alimuomba kuibuliwa, kuimarishwa na kuhifadhiwa majengo na zana zamani za kimila ili kubaki kama kielelezo cha utamaduni wetu pamoja na kuyarejesha nchini mafuvu ya machifu hao.

Akizungumzia maombi hayo, Rais Samia amesema kuhusu kazi data tayari serikali kwa kushirikiana na umoja wa machifu nchini inaendelea kuwasajili ili kuanzisha kanzi data yao.

“Hadi kufikia 20 Januari, jumla ya machifu 92 tayari wamesajiliwa wakiongozwa juu kule na Chifu Hangaya. Nami pia nimesajiliwa kwenye umoja huo.

“Pia maofisa utamaduni wa mikoa wameagizwa kwa kutumia sifa na vigezo vilivyowekwa kuwatambua machifu na kuwasilisha taarifa zao wizarani,” amesema.

Kuhusu taarifa sahihi za machifu na mchango wao katika kupambana na ukoloni, Rais Samia amesema mbali na taarifa zilizopo sasa idara ya maendeleo ya utamaduni inaendesha programu maalumu ya kuhifadhi taarifa za ukombozi, kupitia program hiyo machifu na viongozi wa kimila wanahojiwa jinsi makabila na uongozi wao walivyoshiriki katika mapambano dhidi ya ukoloni na kupigania uhuru.

“Baadhi ya machifu wa mikoa ya Mbeya na Singida tayari wamehojiwa na kazi inaendelea,” amesema.

Akizungumzia kuhusu mapango yaliyotumiwa na machifu kutambuliwa, Rais Samia amesema mpaka mwezi Januari, maeneo ya mapango 36 yamebainishwa na tathmini ya kina inafanywa ili yaweze kuidhinishwa kama maeneo ya vivutio vya utalii.

Amesema Serikali kupitia wizara ya utamaduni ilishakutana na machifu jijini Dodoma, Oktoba mwaka jana, kwamba pamoja na fursa ya kutoa maoni kwenye sera ya utamaduni.

“Mlikubaliana pia kila chifu awasilishe orodha ya maeneo yaliyopo katika himaya yake na niwahimize machifu wote mfanye hivyo kwa wale ambao bado hawajawasilisha maeneo hayo ili kwa pamoja tutengeneze kanzi data ya kitaifa ya kuwatambua machifu waliopo tuweze pia kuwa na taarifa sahihi za urithi uliopo katika himaya zao,” amesema.

Aidha, kuhusu kuimarishwa na kuhifadhiwa majengo na zana zamani za kimila, Rais Samia amesema hadi sasa zaidi ya majengo 200 ya machifu yenye historia za kiutamaduni tayari yametambuliwa.

“Nimefurahi kusikia leo kuna jengo lingine limeonekana ndani ya mkoa wa Kilimanjaro na wizara watafuatilia na kuiona jinsi ya kuliorodhesha katika orodha ya majengo hayo.

“Pia zana mbalimbali zilizokuwa zikitumiwa nyakati hizo, zimehifadhiwa katika makumbusho ya Taifa, tafiti za kubaini maeneo na zana za aina hiyo zinaendelea,” amesema.

Akizungumzia kuhusu kuyarejesha nchini mafuvu ya machifu yaliyochukuliwa wakati wa ukoloni ili yatumike kuelimisha jamii na shughuli za kitalii amesema watakapofanikiwa, Serikali itatoa taarifa ipasavyo.

Kwa upande mwingine Rais Samia amesema katika kikao cha Dodoma kati ya machifu na wizara ya utamaduni, ilikubalika kuwepo kwa Jukwaa la pamoja baina ya serikali na machifu la kila mwaka ambalo hoja na masuala ya machifu yatajadiliwa na kutolewa ufafanuzi na au kutatuliwa.

“Nataka niwape taarifa machifu wenzangu kwamba jukwaa hili nitaliongoza mwenyewe, niupongeze ubunifu na utayari wa kukutana na nisisitize utaratibu huu tuuendeleze,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *