Saturday , 25 March 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko Mafunzo ya Ualimu Tanzania yaboreshwa, cheti chafutwa
Habari Mchanganyiko

Mafunzo ya Ualimu Tanzania yaboreshwa, cheti chafutwa

Spread the love

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania imeufuta mtaala wa ualimu wa ngazi ya cheti kwa elimu ya awali na msingi na kuanzisha wa Diploma ikwa ni hatua ya kuboresha elimu nchini humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Mtaala huo ulioboreshwa na Taasisi ya Elimu Tanzania kwa ushirikiano na wadau mbalimbali, utawezesha wanaojiunga na mafunzo ya ulimu watasoma kwa miaka miaka mitatu.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu tarehe 5 Oktoba 2020 na Dk. Ave Maria Semakafu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari.

Dk. Semakafu amesema, ulioboreshwa unatoa nafasi kwa mwalimu katika mwaka wa pili wa masomo kuchagua eneo la umahiri atakalobobea tofauti na mfumo wa zamani ambao haukuwa katika muktadha huo.

Amesema, walimu walioko tayari vyuoni wakisoma cheti ambao watamaliza mwaka 2021 hao ndiyo wa mwisho kudahiliwa.

“Mtaala huu mpya utaanza kutumika mwaka wa masomo 2020/21 na mwalimu yeyote mwenye cheti cha ualimu atakuwa na sifa ya kusomea Diploma ya ualimu wa elimu ya awali au msingi na vilevile atakapohitimu na kufaulu atakuwa na sifa ya kujiunga na Chuo Kikuu kupata shahada ya kwanza ya ualimu wa elimu ya awali au msingi,” amesema Dk. Semakafu

Amesema, programu itakayofundishwa itakuwa ya miaka mitatu na kwamba masomo yatafundishwa kwa lugha mbili ambazo ni Kiingereza na Kiswahili kutokana na kuwepo kwa shule za English medium nchini.

“Walimu waliosoma Astashada (cheti bado Serikali inatambua uhitimu wa cheti katika kada ya ualimu na ipo kwenye mfumo wa utumishi na itaendelea kuwepo na hakuna mwalimu atakayefukuzwa kazi kwa kuwa yeye ni mwalimu wa ngazi ya cheti,” amesema

Amesema, kwa walimu walioko kazini watakaopenda kujiendeleza wanaweza kusoma kwa masafa kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) kwa njia ya masafa, njia ambayo haita athiri utendaji na mwisho kufanya mitihani ili kupata Diploma.

“Kwa walimu ambao wana vyeti na hawajaweza kupata fursa ya ajira, watatakiwa kurudi vyuoni na kuweza kupata Diploma ya ualimu,” amesema

Amesema, lengo la maboresho hayo ni kuifanya kada ya ualimu kuheshimika na kuendana na ukuaji wa uchumi wa kati ambayo Tanzania imeifikia.

Dk. Semakafu amesema, “tunafurahi kwamba wenzetu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wataanzisha shahada ya ualimu wa awali na msingi. Lengo ni kuhakikisha tunakuwa na walimu bora zaidi.”

Amesema, sifa za kujiunga na mafunzo ya Diploma zitakuwa zile zile za daraja la kwanza hadi la tatu kwa wahitimu na kidato cha nne na wale wa kidato cha sita.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania , Aneth Komba amesema, “tuneboresha na kuongeza hadhi ya ualimu. Sasa tutakuwa na Diploma na zamani mtakumbuka tulikuwa hatuna shahada ya shule za msingi, lakini tunakwenda kuianzisha.”

“Tunataka kuwafanya kuwa wabobezi na tutaongeza walimu bora zaidi kwa walimu wenye cheti waliopo kazini, tumeandaa programu rafiki ya masafa na watasoma wakiwa kazini na kipindi cha likizo wataweza kukutana vyuoni kwa ajili ya kufanya mitihani,” amesema Aneth

Kuhusu mahitaji ya walimu, Dk. Semakafu amesema, upungufu wa walimu upo wa masomo ya fizikia, hisabati, kilimo na mafunzo ambao Serikali inatarajia kupunguza tatizo hilo kupitia ajira zilizotangazwa na Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Watendaji Kata, Mitaa watakaoshindwa kusimamia usafi kukiona

Spread the love  WATENDAJI wa kata, mitaa na vitongoji na maofisa afya...

Habari Mchanganyiko

Mtia nia urais TLS kukata rufaa kupinga kuenguliwa

Spread the love  MTIA nia ya kugombea Urais wa Chama cha Mawakili...

Habari Mchanganyiko

NBC yazindua kampeni ya mkeka wa ushindi na ATM zake

Spread the loveBENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imetangaza uzinduzi wa kampeni...

Habari Mchanganyiko

Uholanzi wampongeza Rais Samia kuimarisha vyombo vya habari, demokrasia

Spread the love  UBALOZI wa Uholanzi nchini Tanzania, umempongeza Rais Samia Suluhu...

error: Content is protected !!