August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mafundi waililia Tanzania ya viwanda Morogoro

Spread the love

MAFUNDI wa kushona na kuuza viatu Manispaa ya Morogoro wameiomba Serikali kuanzisha viwanda vya ngozi na vya kutengeneza viatu ili kuwafanya kupata malighafi ikiwemo ngozi na soli kwa bei nafuu, anaandika Christina Haule.

Ernest Mhando mmoja kati ya mafundi hao, amesema kwa licha ya kupatikana kwa ngozi kwa sasa lakini madawa ya kuchakatia ngozi hizo hayapo nchini na hupatikana kwa bei ya juu kutoka kwa wauzaji wa bidhaa hizo.

“Tunanunua ngozi kwa bei ya juu ya shilingi 4,000/- kwa futi moja huku kiatu jozi moja kikitumia futi 3, hivyo kiatu hadi kinakamilika kutumia gharama ya shilingi 18,000/- na kuuzwa kwa Sh. 30,000/- bei ambayo wachache sana wanaimudu,” amesema.

Pamoja na kukabiliwa na changamoto ya ngozi pia mafundi hao wanakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa masoko la uhakika ambapo wanunuzi wengi hununua viatu vya plastiki kwani bei yake ni ya chini, inayofikia mpaka Sh. 8,000/-

Aidha amesisitiza kuwa viatu vya ngozi kutoka nje ya nchi vimekuwa na bei ya chini kufikia Sh. 20,000/- hivyo kuvinyima soko viatu vya ndani kutokana na ukosekanaji wa malighafi muhimu kwaajili ya utengenezaji wa viatu.

Elihuruma Mbaga, fundi viatu, Manispaa ya Morogoro yeye ameiomba serikali kuboresha viwanda vya zamani vya ngozi ili kusaidia uchakataji wa ngozi na kupatikana kwa bei nafuu.

“Tunaisubiri Tanzania ya viwanda ili na sisi huku viwepo viwanda vitakavyotuwezesha kutengeneza viatu vyenye ubora ili kupata masoko ya ndani na nje ya nchini,” amesema Mbaga.

Amesema kwa sasa wanategemea ngozi kutoka katika maduka ya wachuuzi ambao hununua kutoka nchi za Zambia na Nairobi.

“Miaka ya 1992 hadi 1998 wakati kiwanda cha ngozi kinafanya kazi hapa, tulikuwa tunanunua futi moja ya ngozi kwa Sh. 350/- sasa hivi tunanunua Sh. 4,000/- kutokana na kukosekana kiwanda,” amesema.

 

error: Content is protected !!