July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mafisadi sasa kumekucha

Spread the love

AHADI ya Rais John Magufuli kuanza kushughulika na viongozi wa umma wanaofanya ufisadi, sasa inapelekwa mkukumkuku, anaandika Faki Sosi.

Ikiwa tayari Bunge la Jamhuri limepitisha Sheria ya Uanzishwaji wa Mahakama nchini, Jukwaa la Haki na Jinai ambalo hujumuisha vyombo vya dola linakutana mjini Dodoma kuanza mchakato huo.

Kauli hiyo imetolewa jana na Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Katiba na Sheria ambapo amesema kuwa, lengo la kikao hicho ni kufanya maandalizi ili khakikisha mahakama hiyo inafanya kazi zake kwa ufanisi.

Kikao hicho kinahitimishwa leo ambapo amesema, washiriki wake ni wale alio katika taasisi za haki jinai.

Taasisi zilizotajwa ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Usalama wa Taifa na Jeshi la Polisi.

Na kwamba, Takukuru wanapaswa kufanya uchunguzi kwa haraka, polisi watatakiwa kupeleleza haraka na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) atatakiwa kufanya kazi kwa ufanisi.

Hatua ya kuelekea uanzishwaji wa mahakama hiyo ni ahadi ya Rais Magufuli kuahidi uanzishwaji wake wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana.

Hivi karibuni, Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu alilieleza Bunge kuwa, tayari serikali ilianzisha Divisheni ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi katika Mahakama Kuu.

“Kuhusu ahadi ya kuanzisha Mahakama Maalum ya Ufisadi napenda kuliarifu Bunge lako kwamba, Serikali imeanzisha Divisheni ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi katika Mahakama Kuu itakayoanza kufanya kazi mwezi Julai 2016,” amesema Majaliwa.

Aliahidi kuwa, serikali itaimarisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kwa pamoja ziweze kuharakisha utoaji wa haki kwa kesi zitakazofikishwa kwenye mahakama hiyo.

Kiongozi huyo wa serikali aliongeza: “Serikali itaimarisha ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kwa pamoja ziweze kuharakisha utoaji wa haki.”

Katika siku ya kilele cha Wiki ya Mwaka Mpya wa Mahakama Jijini Dar es Salaam mapema mwaka huu, Rais Magufuli alimtaka Jaji Mkuu, Othman Chande kutosubiri Bunge kupitisha Sheria ya Uanzishwaji wa Mahakama ya Mafasidi, badala yake mahakama hiyo ianze kufanya kazi haraka iwezekanavyo.

Amesema, kuchelewesha kuanza kwa mahakama hiyo kunatoa mwanya kwa mafisadi kuendelea kuangamiza nchi na kuifanya kuwa masikini wakati ina rasilimali za kutosha ambazo zinaweza kuiendesha nchi bila kutegemea fedha za wafadhili.

error: Content is protected !!