August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mafisadi CDA kuisoma namba

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, George Simbachawene

Spread the love

WALIOKUWA wafanyakazi waandamizi wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), huenda wasipangiwe majukumu mapya katika idara na mamlaka za umma, iwapo baadhi yao watathibitika kuhusika na vitendo vya ufisadi na kujilimbikizia mali, anaandika Dany Tibason.

Mtandao wa MwanaHALISI online umedokezwa kuwa hatua hiyo inatokana na malalamiko ya maandishi yaliyowasilishwa na baadhi ya wananchi kwenye mamlaka mbalimbali za nchi juu ya utendaji wa baadhi ya waliokuwa maofisa wa juu wa CDA.

Chanzo chetu kimetueleza kuwa kutokana na taarifa za tuhuma za ufisadi wa vigogo hao wa CDA kusambaa kwenye mamlaka za juu kwa sasa Godwin Kunambi, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Dodoma, amewapangia kazi baadhi ya waliokuwa watumishi wa CDA tu lakini waliokuwa viongozi wa juu wamewekwa kando.

“Mkurugenzi Kunambi, hajawapangia kazi vigogo wa CDA, anasubiri maelekezo kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), George Simbachawene ili aweze kuambiwa hatua za kuchukua dhidi yao,” kimeeleza chanzo chetu.

MwanaHALISI online lilipomtafuta Kunambi, alisema, “Naomba ufanye subira, kwa sasa tumeanza kuwapangia kazi baadhi ya wafanyakazi kutoka CDA, lakini waliokuwa watendaji waandamizi bado.

“Si kwasababu ya hicho unachokisema ila ni utaratibu tu tunaoletewa kutoka mamlaka za juu,” alisema Kunambi.

Tarehe 15 Mei mwaka huu, Rais Magufuli alitangaza kuivunja rasmi CDA na kuamuru shughuli zilizokuwa zikifanywa na mamlaka hiyo zihamishiwe katika Manispaa ya Dodoma, na kwamba wafanyakazi wa CDA watapangiwa kazi zingine katika idara za serikali.

error: Content is protected !!