Thursday , 30 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Mafao ya wastaafu: Magufuli awanyooshea kidole mawaziri “hamuwasiliani”
Habari za SiasaTangulizi

Mafao ya wastaafu: Magufuli awanyooshea kidole mawaziri “hamuwasiliani”

Spread the love

 

TATIZO la wastaafu nchini Tanzania, kuchelewa kulipwa mafao yao, linasababishwa na baadhi ya mawaziri kutowajibika ipasavyo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa tarehe 26 Februari 2021, na Rais John Magufuli, wakati anazungumzia changamoto ya baadhi ya wastaafu wa Jeshi la Polisi, kuchelewa kulipwa mafao yao.

Amesema hayo, baada ya kumaliza kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kiwanda cha Ushonaji katika Bohari Kuu ya Jeshi la Polisi na kuzindua majengo ya ofisi, madarasa pamoja na bweni la wanafunzi, Chuo cha Taaluma ya Polisi, Dar es Salaam.

Rais Magufuli amesema, mawaziri hao wasiowajibika ndiyo wanaosababisha matatizo ya watumishi kumaliza muda wao wa utumishi na kuanza kusotea mafao yao.

“Tatizo la mawaziri wangu hamu- communicate (hamuwasiliani, mnaleteleza watu wa chini kupata shida, huu ni wajibu wa wizara ya mambo ya ndani. Nikificha ni unafiki,” amesema Rais Magufuli.

Ametoa ufafanuzi huo, baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, kumuomba atatue changamoto ya baadhi ya wastaafu wa jeshi la polisi, kuchelewa kulipwa mafao yao.

Amiri Jeshi Mkuu huyo amesema, Simbachawene alipaswa kupeleka orodha ya majina ya wastaafu hao wizara ya fedha, badala ya kubaki ofisini, “msema kweli ni mpenzi wa Mungu, nawashangaa ninyi wizara ya mambo ya ndani.”

“Mstaafu wako amefanya kazi yake nzuri, amemaliza bila tatizo lolote, anatakiwa kulipwa mafao yake na yapo, waziri unakaa ofisini bila kwenda kuwaombea kwa nini?”

“Katibu mkuu na naibu katibu mkuu unakaa ofisini. Kwa nini usichukue majina ukatembea wizara ya fedha ukasema nina wastaafu hawa nataka fedha zao,” amehoji Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, hata yeye alipokuwa waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano, alikuwa anaisumbua wizara ya fedha kulipa fedha za wakandarasi.

“Wakati nikiwa waziri wa ujenzi, nikipata shida ya makandarasi, nilikuwa naenda kufanya fujo wizara ya fedha, nataka hela za wakandarasi na hela zinalipwa. Sasa hii wizara wastaafu wenu wanamaliza kazi, hamuwezi kwenda kugombana kupata hela” amehoji Rais Magufuli.

Kufuatia changamoto hiyo, Rais Magufuli amewataka wastaafu wa jeshi hilo waliochelewa kulipwa mafao yao, kumlaumu Waziri Simbachawene na watendaji wengine katika wizara hiyo, akiwemo Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro.

“Hili ni tatizo la wakubwa wenu wizarani, sitaki kusema kwa unafiki, mbona jeshini hawanisubiri mimi wakistaafu? Ninyi wastaafu wa polisi, muwalaumu Waziri Simbachawene, IGP, katibu mkuu wake, naibu katibu na wakurugenzi sababu hawapigi kelele,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesisitiza “wakitaka wastaafu kulipwa watalipwa wala haitachukua siku tano. Hii ni changamoto kwenu viongozi wakubwa wa wizara wala mimi msiniambie, nyie mniambie waziri amekataa kutoa hela, ili mimi nimlazimishe kutoa hela kwa nguvu.”

Kiongozi huyo wa nchi, amemuagiza Waziri Simbachawene kufuatilia mafao ya wastaafu hao, ili walipwe ndani ya wiki moja.

“Nakuagiza, nenda kashughulikie malipo ya wastaafu na ikiwezekana ndani ya wiki moja wawe wamelipwa, tuliwatumia vizuri kabla hawajastaafu tuwalipe vizuri mafao yao,” amesema Rais Magufuli

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

TEMESA iliyokarabati Kivuko kwa Bil 7.5 yapata hati chafu

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

ACT-Wazalendo yakusanya Mil 8.5/- kodi ya zuio na kutokomea nazo

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

DC Kasilda Mgeni ahamasisha chakula shuleni

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni...

Habari za Siasa

Bilioni 223.9 zapelekwa Tunduru ndani ya miaka 2 ya SSH

Spread the love  ZAIDI ya Sh. bilioni 223.9 zimepelekwa Wilaya ya Tunduru...

error: Content is protected !!