November 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maelfu wajitokeza kumlaki Dk. Mengi

Spread the love

MAELFU ya watu jijini Dar es Salaam, wamejitokeza kuupokea mwili wa aliyekuwa mwenyekiti wa kampuni ya Industrial Projects Promotion (IPP Limited), Dk. Reginald Abraham Mengi. Anaripoti Hamis Mguta … (endelea).

Mwili wa Dk. Mengi, uliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, majira ya saa 9:20 alasiri.

Kabla ya kupelekwa kwenye hospitali ya jeshi ya Lugalo kuhifadhiwa, mwili wa marehemu Dk. Mengi ulisimamishwa kwenye lango kuu la kutolea mizigo kwa ajili ya swala.

Katika tukio hilo, mamia ya waombelezaji waliopata bahati ya kuingia ndani ya eneo hilo, walibubujikwa na machozi ishara ya kumlilia mpendwa wao.

Dk. Mengi alikutwa na mauti usiku wa Jumatano, akiwa Dubai, Falme za Kiarabu alipokwenda kwa mapumziko ya baada ya pasaka.

Katika uwanja wa ndege, mwili wa marehemu Dk. Mengi, ulilakiwa na watu mbalimbali, akiwamo mtoto wake, Abdiel Mengi; aliyekuwa waziri wa mambo ya nchi za nje katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete, Bernard Membe na waziri wa mifugo na uvuvi, Luhaga Mpina.

Wengine, ni mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema katika jimbo la Ubungo, Saed Kubenea; mbunge wa kuteuliwa, Mama Salma Kikwete; mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na mkuu wa mkoa wa Njombe, Christopher ole Sendeka.

Katika orodha hiyo, wamo pia mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi na mbunge wa Vunjo, James Mbatia; wakili mashuhuri wa mahakama kuu na mwanasheria wa familia hiyo, Michael Ngalo na Kanal mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Joseph Simba Kalia.

https://www.youtube.com/watch?v=szTLPNPZrx8

Marehemu Mengi alisindikizwa kutoka Dubai kuja Dar es Salaam na mtoto wake, Regina, mdogo wake, Benjamin Mengi, mke wake Jacqueline Ntuyabaliwe na balozi wa Tanzania katika nchi za Falme za Kiarabu, Mbarouk Nassor Mbarou.

Dk. Mengi alizaliwa katika kijiji cha Machame, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, tarehe 29 Mei mwaka 1942, akiwa mmoja wa watoto saba wa Bw. Abhraham Mengi na Bi Ndeekyo Mengi.

Alianza safari yake kielimu katika Shule ya Msingi, Kisereny Village na  Bush School, kabla ya kujiunga Nkuu District School na baadaye Siha Middle School.

Alijiunga na Old Moshi Secondary School na kwa ufadhili wa Chama cha Ushirika kilichokuwa na nguvu ya kifedha – Kilimanjaro National Cooperative Union (KNCU) – Dk. Mengi, aliweza kusomeshwa masomo yake ya shahada ya kwanza ya uhasibu nchini Uingereza.

Baada ya masomo ughaibuni, Mengi alirudi Tanzania 1971 na kuajiriwa na kampuni ya Cooper and Lybrand Tanzania (sasa Prince water house Cooper) mpaka mwaka 1989 alipoamua kujikita kwenye ujasiriamali.

Dk. Mengi alinukuliwa mara kadhaa akisema, “nimetoka katika familia ya kimasikini sana. Kila siku ilikuwa ni vita ya kupambana na umasikini. Tulimiliki sio zaidi ya ekari moja, tukiishi kwenye vibanda vya udongo tukichanganyika na ng’ombe wachache na kuku.

“Ninaporudisha fikra na kutazama nyuma ni vigumu napatwa na ugumu wa kufikiri namna tulivyoweza kuishi katika hali ile.”

Ni jambo hilo pia ndilo lilomsukuma kuchapisha kitabu cha maisha yake mwaka 2018 kiitwacho I can, I must, I will (Ninaweza, Lazima nifanye, Nitafanikisha) kinachoangazia historia ya maisha yake toka alipozaliwa mpaka kufanikiwa kibiashara.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na familia, kesho mwili wa Dk. Mengi utafikishwa kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa nafasi kwa wananchi kutoa salamu zao za mwisho.

Kutoka Karimjee, mwili wake utaletwa nyumbani kwake Kinondoni; Jumatano utasafirishwa kupelekwa nyumbani kwake Machame, na  ibada ya mazishi itafanyika katika Kanisa la Kilutheri la Kiinjili Tanzania la Kisereni, jijini Moshi.

Kupitia IPP Limited, Dk. Mengi alianzisha makampuni mbalimbali na kufanya biashara kadha, ikiwamo uzalishaji wa kalamu, sabuni, soda, maji ya kunywa, madini, mafuta, gesi asilia na kilimo.

Hata hivyo, umaarufu mkubwa wa Mengi ni kutokana na kumiliki vyombo vya habari, kuanzia magazeti, vituo vya runinga na redio. Runinga yake ya ITV pamoja na kituo cha Redio One ni moja ya vituo vikubwa vya utangazaji huku magazeti yake ya Guardian na Nipashe yakiwa miongoni mwa magazeti makubwa zaidi Tanzania.

Mpaka umauti unamfika, Mengi alikuwa mwenyekiti wa Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo Vya Habari Tanzania (MOAT).

Dk. Mengi amekuwa akijitoa katika kusaidia wasionacho na wenye uhitaji kwenye jamii ikiwemo walemavu wa ngozi na kugharamia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo nchini India.

Mwaka 2014, jarida maarufu la masuala ya fedha Forbes lilikadiria utajiri wa Mengi kuwa unafikia dola milioni 560.

Dk. Mengi anatarajiwa kupumzishwa kwenye nyumba yake ya milele huko Machame, siku ya Alhamisi.

error: Content is protected !!