March 6, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Madudu yabainika Viwanja vya ndege

Ujenzi wa Uwanja mpya wa Julius Kambarage Nyerere

Spread the love

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali imemwagiza Mkaguzi na Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), anaandika Dany Tibason.

Kamati hiyo imetoa agizo hilo baada ya kubaini kuwepo kwa mapungufu mengi katika taarifa zao za fedha.

Agizo hilo lilitolewa jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka baada ya kamati hiyo kupitia ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha 2015/2016.

Kutokana na kuwepo kwa mashaka na mwenendo wa matumizi ya Mamlaka hiyo kamati imemwagiza CAG afanye ukaguzi maalum wa shughuli zote za kiuhasibu za TAA na waangalie watumishi wa idara ya fedha na wakurugenzi kama wanatosheleza ama la.

Mwenyekiti huyo amesema CAG atakapomaliza ukaguzi maalum waiwasilishe ripoti hiyo kwa Katibu wa Bunge.

Kaboyoka ambaye pia ni Mbunge wa Same Mashariki (Chadema) aliagiza bodi ifuatilie mapendekezo yote yaliyotolewa ndani ya ripoti ya CAG na kuiwasilisha ofisi ya CAG.

Awali wabunge walisema kuwa taarifa za fedha za mamlaka hiyo zimepingwa na kwamba hazijafuata vigezo vya kisheria na mwongozo wa kimataifa.

Mbunge wa Vwawa (CCM) Japheth Asunga alisema kuwa hesabu za mamlaka hiyo zina mapungufu makubwa hali inayotia mashaka walipataje hati safi.

“Haieleweki hawa wenzetu hata hiyo hati safi wameipataje kwa mahesabu haya yenye mapungufu mengi,”amesema

Mbunge wa Magomeni (CCM) Jamal Kassim amesema kuwa taarifa hizo ni za kupikwa na hawastahili hata kupewa hati safi.

“Ukiangalia ripoti hii utagundua kuwa hesabu hizi ni za kupikwa, wameweka taarifa za kifedha wanazojua wenyewe,”amesema

Baadhi ya wabunge walihoji kuhusu utata wa umiliki wa Kampuni ya Maendeleo ya Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (Kadco).

error: Content is protected !!