August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Madiwani ‘wamshika uchawi’ DC Nyamagana

Mary Tesha, Mkuu wa Wilaya (DC) Nyamagana

Spread the love

MARRY Tesha, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, ameingia katika mvutano na madiwani wa halmashauri ya jiji hilo baada ya kutothibitisha matumizi ya Sh. 100 milioni, alizoomba ili kuwaondoa wafanyabiashara ndogondogo (machinga) kutoka katikati ya jiji, anaandika Moses Mseti.

Madiwani hao wamedai kuwa DC Tesha aliomba fedha hizo ili kuwaondoa machinga katikakati ya jiji lakini hazijafanya kazi hiyo na wala hakuna taarifa za matumizi yake.

Inadaiwa kuwa DC Tesha Sh. 100 milioni ikiwa ni maaazimio ya kikao cha mdiwani kilichofanyika tarehe 5 Agosti, mwaka huu ambapo madiwani walielezwa na Mkurugenzi wa jiji kuwa ofisi ya mkuu wa wilaya imeomba fedha hizo ili kukarabati maeneo watakayopelekwa machinga pamoja na posho za kuwalipa mgambo na askari polisi.

Madiwani walioongea na MwanaHALISI Online huku wakiomba kuhifadhiwa kwa majina yao kwa sasa, wamesema licha ya fedha hizo kutolewa lakini mpaka sasa maeneo hayo hayajarekebishwa na zoezi hilo limesimama baada ya Rais John magufuli kupiga marufu kuondolewa kwa machinga hao.

Wanamshutumu DC Tesha na Mkurugenzi wa jiji hilo kugawana fedha hizo huku wakishanga kuona mkuu wa wilaya hiyo akiomba tena Sh. milioni 113 kwa ajili ya kazi ile ile ya kuwaondoa machinga.

“Mwezi huu tumekaa kikao cha dharura, ajenda ikiwa ni kuwaondoa machinga mjini na tumeambiwa inahitajika Sh. 113 milioni. Tulipojaribu kuhoji fedha za awali zimefanya kazi gani? hatukupewa majibu ya kuridhisha. Tutatoaje fedha wakati za awali hatufahamu zilivyotumika?” amehoji diwani mmoja.

Imeelezwa kuwa madiwani hao wamegoma kuidhinisha fedha zingine kwa DC Tesha, baada ya kukosekana kwa maelezo sahihi ya namna fedha za awali zilizvyotumika.

Maeneo yanayodaiwa kutaka kukarabatiwa ni Community Center (Mirongo), Sinai (Mabatini) na Maduka tisa (Nyasaka).

Tesha alipotafutwa ili kuzungumzia suala hilo kupitia simu yake ya mkononi, iliita na kukatwa na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) katika simu yake ya kiganjani mnamo saa 12:04, uliosomeka;

“Kuna madai kwamba ofisi yako iliomba milioni 100 kutoka halmashauri ya jiji ili kuwaondoa machinga katikati ya jiji, lakini fedha hizo zinadaiwa kutojulikana matumizi yake nabadala yake umeomba tena kiasi cha Sh. 113 milioni kwa kazi hiyo. Je ukweli wa jambo hili upoje?” Ujumbe haukujibiwa mpaka tunaenda mitamboni.

Kiomoni Kibamba, Mkurugenzi wa jiji la Mwanza alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, amesema jiji lilitumia zaidi ya Sh. 20 milioni kukarabati baadhi ya maeneo wanayotaka kuwahamishia machinga hao.

Kibamba alikiri kiasi hicho cha fedha kutengwa na baraza la madiwani, kwa ajili ya kazi ya oparesheni ya kuwaondoa machinga mjini huku akidai kwamba hakuna fedha zilizoliwa.

“Wahoji vizuri madiwani, wakueleze juu ya hizo fedha. Hakuna fedha iliyoombwa tena ili kuwaondoa machinga.

“Pesa iliyotumika inajulikana na iliyobaki ipo, nashangaa kusikia fedha eti fedha zimeliwa na jiji, ingawa ni kweli DC (Marry Tesha) aliomba fedha kuwalipa posho askari, wakati wa oparesheni,” amesema Kibamba.

Kibamba amesema kuwa kiasi cha Sh. 100 kwa ajili ya kuwaondoa machinga si kubwa kwani hapo awali  jiji hilo, chini ya Adam Mgoyi mkurugenzi aliyepita, liliomba Sh. 200 milioni kwa ajili ya kazi hiyo na madiwani walipinga na kukubaliana kuidhinishwa Sh. 100 milioni pekee.

error: Content is protected !!