May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Madiwani Tanzania watangaziwa neema

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imependekeza kuanzia mwaka wa fedha 2021/22, itaanza kuwalipa madiwani posho za kila mwezi kutoka serikali kuu. Anaripoti Jemima Samwel, DMC…(endelea).

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, tarehe 10 Juni 2021 na Dk. Mwigulu Nchemba, alipokuwa anawasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/22, bungeni jijini Dodoma.

Amesema, madiwani wenzetu wanafanya kazi nzuri sana za kusimamia shughuli za maendeleo kwenye kata zetu.

“Hawa ni wabunge wakaazi wa kwenye kata zetu ambao kila siku wako na wananchi wetu kwenye kusimamia shughuli za maendeleo.”

“Hata hivyo, katika baadhi ya halmashauri madiwani wamekuwa wakikopwa posho zao, na wengine hufikia hatua ya kupiga magoti kwa wakurugenzi watendaji ili walipwe,” amesema

Amesema, hali hii imekuwa ikipunguza ufanisi katika halmashauri zetu kwa madiwani wengi kufanya maamuzi yanayopendekezwa na wakurugenzi watendaji hata kama hayana maslahi kwa Taifa ili waweze kulipwa posho zao.

Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango

Waziri huyo amesema, jambo hilo limeongelewa kwa hisia kali sana na waheshimiwa wabunge hapa bungeni.

“Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Madiwani, napenda niwaeleze kuwa Mama yetu amesikia kilio chenu na alinielekeza mimi pamoja na Waziri wa TAMISEMI kulitafutia ufumbuzi suala hili,” amesema

Huku wabunge wakishangilia, Dk. Mwigulu amesema “napendekeza kuanzia mwaka 2021/22, Serikali Kuu ianze kulipa posho za kila mwezi za Madiwani moja kwa moja tena kwenye akaunti zao kwa Halmashauri zote zenye uwezo mdogo kimapato.”

Kuhusu halmashauri 16 zenye uwezo mkubwa wa kimapato (Daraja A) , Dk. Mwigulu amesema “zitaendelea kutumia mapato yake ya ndani kulipa posho za Madiwani kupitia kwenye akaunti zao.”

error: Content is protected !!