August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Madiwani Kinondoni kuvaana ugawaji manispaa

Spread the love

KIKAO cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kimeketi muda huu kujadili ugawaji wa manispaa hiyo ili kupatikana kwa manispaa mpya ya Ubungo, anaandika Regina Mkonde.

Boniface Jacob, Meya wa Manispaa ya Kinondoni amesema anaamini wajumbe wa baraza hilo wataweka masilahi ya wananchi mbele na kuachana na mivutano ya kisiasa.

“Leo (mchana) tunafanya kikao maalum cha baraza kwa ajili ya kupitia mapendekezo ya mgawanyo wa halmashauri ya manispaa ya kinondoni ambapo katika mgawanyo huo Kinondoni itazalisha halmashauri ya manispaa ya ubungo,” amewambia madiwani na kuongeza;

“Kikao hiki cha baraza kina masilahi makubwa kwa wananchi wetu pamoja na halmashauri ya Kinondoni kwahiyo wote lazima tujione kwamba tupo kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi wetu, sitegemei kuona mivutano isiyo na tija.”

Kikao hicho kinatarajia kufanya mgawanyo wa wa mali, rasilimali na madeni ya halmashauri ya Kinondoni ili baadaye kila halmashauri (Ubungo na Kinondoni) ikaanze upya.

Aron Kagurumjuli, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni amesema kikao hicho kimeketi baada ya kamati ya kugawa halmashauri hiyo kukaa vikao na kufikia makubaliano kadhaa ambapo katika kikao cha leo yatajadiliwa na kupitishwa rasmi.

Kikao hicho ambacho huenda kikawa na mvutano mkali baina ya madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa upinzani kufuatia mvutano wa kugawana mali na rasilimali pamoja na madeni kitafanyika bila uwepo wa wandishi wa habari.

Mwaka jana, serikali ilichukua uamuzi wa kuigawa wilaya ya Kinondoni na kuanzisha wilaya mpya ya Ubungo, uamuzi ambao umesababisha kuanzishwa pia kwa Manispaa mpya ya Ubungo ambayo itakuwa na majimbo ya Ubungo na Kibamba.

error: Content is protected !!