August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Madiwani halmashauri Shinyanga wanusa ufisadi

Spread the love

KIKAO cha Baraza la Mmadiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kimevunjika baada ya kukosekana kwa taarifa ya mapato na matumizi katika sekta zote za miradi ya maendeleo, anaandika Mwandishi Wetu.

Baraza hilo lilikutana kwenye kikao cha kawaida cha robo ya mwaka, ambacho kimedaiwa kilipaswa kuwepo na ajenda ya kusomewa taarifa ya mapato na matumizi katika sekta zote za miradi ya maendeleo, ili kufahamu mapato ya halmashauri yapoje na fedha zimetumikaje.

Akitoa hoja kwenye kikao hicho, diwani wa kata ya Mwawaza, Juma Nkwabi, alisema haoni umuhimu wa baraza hilo kuendelea na kikao chake kwa kuwa hakina ajenda.

“Kimsingi ukusanyaji wa mapato ndiyo roho ya halmashauri, ambapo tunapaswa kujua tumekusanya kiasi gani cha pesa na kimetumikaje, ianishwe fedha ya kila mradi kwa sekta zote kuwa zilitengwa kiasi gani, na zimetumikaje ili tujue tukoje na kubaini wapi tumeanguka, na siyo kufichwa,”alisema Nkwabi

Aliongeza kuwa madiwani wote ni wajumbe wa halmashauri, hivyo wanapaswa kujua fedha zinatumikaje kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na kufahamu sekta zingine utendaji wake kazi ukoje huku akitolea mfano kwenye kamati za afya, na miundombinu, lakini cha ajabu wamefichwa taarifa hiyo, na hawajui chochote juu ya matumizi ya fedha hizo.

Diwani wa Kata ya Ndembezi, David Nkulila, alisema kamati yake ya afya ilitengewa Sh. biloni 3.3, lakini hawajui zimefanya kazi gani na hakuna taarifa yoyote ya utendaji kazi, hali ambayo iliwafanya madiwani wote kuazimia kuvunja baraza hadi pale watakapopewa na kusomewa taarifa hizo za mapato na matumizi kwa sekta zote.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Geofley Mwangulumbi, alisema kisheria Madiwani wamekosea kuvunja baraza hilo, ikiwa taarifa zote za miradi ya kusomewa mapato na matumizi hufanyika kwenye mkutano mkuu wa mwaka, mara baada ya kukamilika kwa taarifa hiyo (Finacial Report) ndiyo hutolewa hadharani, na siyo kwenye hicho kikao.

Amesema hajui ni lini ataitisha kikoa cha baraza hilo mpaka atakapopata idhini ya ya Mkuu wa mkoa, Zainabu Telack.

error: Content is protected !!