RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amemwagiza Waziri wa Madini, Doto Biteko kukaa na wawekezaji ili kuangalia njia bora ya kuyalinda madini ya Tanzanite yanayopatikana nchini humo pekee dunia nzima. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).
Samia ametoa agizo hilo leo Jumapili, tarehe 13 Juni 2021, katika siku ya kwanza kati ya tatu ya ziara yake mkoani Mwanza, alipokuwa akifungua Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu.
“Nimeingia ndani nimeoneshwa kiwanda cha kusafisha dhahabu-Mwanza kinavyofanya kazi, kwa maneno mengine ni miujizi, nimeonyeshwa unavyofanya kazi ni dakika tatu,” amesema.
Katika maelezo yake, Rais Samia amesema, “tudhibiti wizi na utoroshaji wa magendo ya madini yetu hususan kwenye migodi yetu ya dhababu na waziri (Biteko), kwenye mgodi wa Tanzanite.”
“Mungu aliipendelea Tanzania pekee akaipa Tanzanite, lakini tunavyokwenda sasa hivi, ni kama inachimbwa dunia nzima, ukienda kwa majirani zetu, Asia yapo. Nimesema, rasilimali zetu, zinakwenda na kumalizika kwa hiyo Tanzanite yetu inaweza kumalizika,” amesema.
Rais Samia amesema, “kuna haja ya kuwa na shirika la kudhibiti Tanzanite yetu, kuwa Tanzanite yote iliyoko mkononi imilikiwe na huyu, nikuombe sana Waziri, kaa na wawekezaji kwenye sekta hii ili kuona jinsi ya kuilinda Tanzanite yetu.”

Pia, Rais Samia maagizo kwa wizara ya madini kuhakikisha “inafuatilia watu waliochukua maeneo lakini hawayaendelezi, ule mtindo wa tajiri mmoja kuchukua maeneo lakini hayaendelezi, naomba liishie hapa.”
Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alisema, kiwanda hicho, kilichozinduliwa kilianza kujengwa 15 Machi 2020 na kukamilika Machi 2021, kikiwa kimegharimu Sh.12 bilioni.
Leave a comment