January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Madereva wapangua kihunzi cha kwanza

Mabasi yakiwa yameegeshwa kwenye kituo cha mabai cha Ubungo baada ya madereva kugoma

Spread the love

HATIMAYE Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani limesalimu amri na kuifuta kanuni ya kuwataka madereva wa magari ya abiria kurudi darasani baada ya miaka mitatu na kupimwa afya zao. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Hatua hiyo imekuja baada ya madereva kuipinga kanuni hiyo kwa mgomo na hivyo, Serikali kulazimika kuunda Tume ya pamoja na wadau wa usafiri ili kujadili na kutatua masuala ya madereva.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani, Mohamed Mpinga, amesema tume imeamua kufuta kanuni hiyo kwa mwaka huu, kutokana kwamba mitaala ya mafunzo hayo haijakamilika.

“Licha ya kuwa mchakato wa kuandaa kanuni hii ulianza tangu mwanzoni mwa mwaka 2014 na kupitia kwa wadau mbalimbali lakini bado hakuna chuo chochote wala ada iliyoainishwa na serikali kwa ajili ya madereva,” amesema Mpinga.

Kuhusu ada iliyokuwa imetamkwa mwanzo na viongozi mbalimbali ya Sh. 560,000, sio sahihi na kwamba serikali haiitambui.

“Tume bado inaendelea na marekebisho ya madai mengine, haswa suala la mshahara na mikataba na baada ya kutatua tutawataarifu madereva na kwamba kuazia sasa hakuna usumbufu wowote utakaojitokeza,” amesema.

Aidha, Mpinga amesema suala la leseni ambazo zimeisha au zitaisha kipindi hiki madereva watabadilishiwa leseni zao kama kawaida kwa utaratibu ule wa zamani pasipokuulizwa vyeti vya mafunzo.

Neye Mwenyekiti wa umoja wa madereva Tanzania, Clement Masanja amewataka madereva wote kuwa wavumilivu kwa matatizo na changamoto zao kwani kamati ya kudumu iliyoundwa itawapatia ufumbuzi.

“Naomba kwanzia sasa tuwe na amani na tuifanye kazi yetu kwa uangalifu kwa kufuata kanuni za usalama barabarani ili kuepukana na ajali za mara kwa mara. Pia namshukuru Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa kuunda kamati hii tunatumaini itatatua matatizo yetu kwa amani,” amesema Masanja.

error: Content is protected !!