September 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Madereva mwendokasi waendeleza mgomo

Spread the love

HUDUMA ya usafiri inayotolewa na mabasi yaendayo kwa kasi jijini Dar es Salaam ipo shakani kufuatia madereva wa mabasi hayo kuendeleza mgomo wakilalamikia kile wanachokiita mkataba ‘tata’ waliopewa, anaandika Hamisi Mguta.

Madereva hao waliogoma kusaini mkataba waliopatiwa 11Juni mwaka huu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo jina la kampuni kutumika ‘UDA’ badala ya ‘UDA-RT’ wameendelea kushikilia msimamo wao mpaka pale madai yao yatakapopatiwa ufumbuzi.

Ramadhani Maulid, dereva wa moja ya mabasi hayo amesema mkataba wa kwanza uliotolewa Januari mwaka huu na kampuni hiyo ulikua na jina la UDA-RT lakini walikataa kuusaini kutokana na mshahara mdogo uliotajwa!

“Wanasema mshahara wa dereva ni Shilingi laki nane, halafu katika mshahara huo laki nne ni lazima kuipata lakini fedha inayobaki hatupati kama hujatimiza vigezo vya ufanisi wa kazi. Hakuna mshahara wa aina hii.” Amesema Ramadhan.

Dereva mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Hassan ameionyesha Mwanahalisi online nakala ya mkataba huo uliosomeka ‘UDA MANAGEMENT AGENCY LIMITED’ huku akisema; “Ni lazima tuelezwe kwanini wamebadili jina?”

Dereva huyo amesema kuwa hawajui mwajiri wao ni nani kwasababu wamepewa mkataba wenye jina la kampuni tofauti na wanayoifahamu.

Wakati huo huo dereva aliyejitambulisha kwa jina moja la Omary, amesema tangu kuanza kwa mgomo huo, uongozi wa kampuni hiyo hautaki kuonana nao wala kuwasikiliza na kila mara umekuwa ukiwakwepa’.

Jumla ya madereva 62 tayari wamesimamishwa kuendelea kuendesha magari hao kufuatia mgomo huo ambapo mtandao huu umeona notisi yenye tangazo la kuwasimamisha madereva hao pamoja na majina yao.

Akijibu hoja za madereva hao, David Mgwassa, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo amekiri kuwepo kwa utata katika mikataba ya madereva hao ikiwemo mgawanyiko wa kupokea nusu ya mshahara na nusu nyingine kufuatia baadaye.

“Fedha atakazolipwa dereva ni kiwango kisichobadilika ambacho ni laki nne lakini kiwango kilichobaki (laki nne pia) ni kiwango kinachotokana na ufanisi kitalipwa kulingana na ufanisi wa kazi kwa kila dereva.” Amefafanua Mgwassa.

Mgwassa amesema mgawanyo huo unatokana na makato ya makosa kampuni yao inakatwa na Dart ambao ndio wakala wa mradi huo.

error: Content is protected !!