January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Madereva mafunzoni siku 5 mfululizo

Spread the love

UMOJA wa Madereva wa Tanzania (UWAMATA) umesema hawatagoma kazi kama inavyoenezwa na wasiowatakia mema kimaslahi, isipokuwa wamepanga kuingia katika mafunzo ili kutekeleza agizo la serikali la Agosti 15 mwaka huu la kuwataka waelimishane. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Serikali kupitia Katibu Mkuu wake Wizara ya Kazi na Ajira, iliandikia uongozi wa UWAMATA barua ikitaka wasigome bali wajikusanye kwenye semina ya kuelimishana taratibu za usalama barabarani.

Barua hiyo imesainiwa na Afisa Kazi katika Wizara hiyo, Omary Sama ambaye amesema madereva wanahitaji mafunzo ya kuwasaidia kuepusha ajali na kuzuia migomo ya mara kwa mara.

Naibu Katibu Mkuu wa UWAMATA ambaye pia ndiye msemaji wao, Rashid Saleh amesema baada ya kumalizika kikao cha mwisho cha majadiliano kati yao na kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kilichofanyika Agosti 13, bila ya muafaka kufikiwa, wameamua kushughulikia agizo la serikali la kuelimishana.

“Tangu kamati iundwe tumekaa mara sita lakini hakuna hata siku moja ambayo tumewahi kujadili changamoto zetu; yaani tukifika pale ni kufungua kikao, tunajadili habari za mizani, miundombinu, usalama barabarani lakini sio madai yetu ya mishahara wala mikataba. Je sisi huku wenzetu wanatuelewaje? Ndo maana wengine walitaka kugoma,” amesema.

“Halafu kamati yenyewe iliyoundwa haina rufaa wala huwezi kushitaki popote. Wanaoendesha ni walewale na wasimamizi ni walewale. Sisi tunamtaka Waziri mwenyewe awepo katika vikao vyetu asikilize hapatikani.”

Waziri Mkuu Pinda aliunda kamati ya watendaji wa serikalini ikiongozwa na Waziri wa Uchukuzi, Samwel Sitta baada ya madereva kulalamika kuwa pamoja na kuwasilisha madai yao serikalini, hakuna hatua iliyochukuliwa kuyafanyia kazi.

Akizungumzia mafunzo watakayokaa kupeana, Saleh amesema yataanza wiki ijayo kupitia Ofisi za Kanda kote nchini, na yatakuwa ya siku nne au tano.

“Tutapata mafunzo ya njia za kuzuia ajali, madhara ya migomo, na elimu nyingine kuhusu udereva. Tayari viongozi wetu wapo katika harakati za kwenda kila mkoa ili kuwaandaa madereva na semina hiyo ambayo imekubaliwa na madereva wote nchini,” amesema.

Amesema wakufunzi watakuwa miongoni mwa madereva wenyewe kwa kuwa wapo wenye elimu nzuri ya masuala yote hayo na watakuwa walimu kwa wale ambao hawajapata mafunzo vya kutosha.

Saleh ametoa mfano wa ushirikiano mdogo wanaopata serikalini kwa kutoandaliwa utaratibu wa kuwawezesha madereva kuandikishwa katika daftari ili nao wapate haki ya kupiga kura wakati utakapofika.

“Hili pia serikali haikuliona kama lina umuhimu, haikutenga muda maalum kwa madereva kwenda kujiandikisha. Sisi kila sehemu ni watu wa mwisho hatuangaliwi tungeacha kazi ili tukajiandikishe tungeambiwa tumegoma.”

Amesema chondechonde serikali isiwasumbue katika siku walizopanga kushiriki mafunzo kwa kuwa wamo katika kutekeleza agizo lao serikali la kuwapa mafunzo.

error: Content is protected !!