August 12, 2022

Uhuru hauna Mipaka

MaDC watakiwa kufanya kazi za CCM

Jakaya Kikwete

Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa CCM aliyemaliza muda wake

Spread the love

Serikali imetakiwa kutoa semina kwa wakuu wa Wilaya wapya hapa nchini ili waweze kuelewa majukumu yao ikiwemo kukijenga na kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika maeneo yao ya utawala, anaandika Regina Mkonde.

Hayo yamesemwa hii leo na Rais mstaafu wa awamu ya nne Dk. Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa CCM ambaye amemkabidhi kijiti hicho Rais John Pombe Magufuli katika mkutano mkuu wa chama hicho mkoani Dodoma.

“Wakuu wa mikoa na wilaya ambao ni wapya wanahitaji semina, wengi ni wasomi na wataalamu ambao mambo ya siasa hawayafahamu vizuri, wanatakiwa kujua wao ni viungo muhimu katika ujenzi wa chama na wakikumbushwa hili mapema itakuwa vizuri.” amesema Kikwete.

Wito wa Kikwete kusisitiza wakuu wa wilaya na mikoa hapa nchini kutakiwa kuijenga CCM katika maeneo yao umezua mjadala mkubwa kwani baadhi ya wateule katika nafasi hizo ni wanajeshi wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) ambao bado hawajastaafu.

Kikwete, mwenyekiti aliyemaliza muda wake leo pia amemuasa Rais Magufuli kama mwenyekiti mpya wa CCM taifa kuendelea kukijenga na kukiimarisha chama katika vyuo vikuu hapa nchini ili kuifuta dhana kuwa chama hicho hakikubaliki kwa wasomi.

“Mwanzoni ilijengeka dhana kuwa huko vyuoni kuwa ccm haitakiwi, eti vinatakiwa vyama vya upinzani tu lakini tulijijenga na kuanzisha shirikisho la vyuo vikuu ili kuiondoa hii dhana na ni vyema kazi hii nzuri ikaendelezwa.” amesema.

Katika hatua nyingine Kikwete amewataka wanachama wa CCM kote nchini kuwaunga mkono Dk. Magufuli na Dk. Shein ili waweze kufanya vyema kazi za serikali.

“Ni wajibu wetu ndani ya chama kuwaunga mkono marais wetu wawili, rais wa Jamuhuri na rais wa Zanzibar kwa jitihada kubwa wanazofanya katika kutuletea maendeleo. Amesisitiza Kikwete.

error: Content is protected !!