October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maboresho Hospitali ya Rufaa Tanga yawafuta machozi wananchi

Spread the love

IMEELEZWA kuwa Serikali imejibu kilio cha muda mrefu cha watumiaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma za kusafisha damu katika hospitali hiyo. 

Hatua hiyo imekuja baada ya hospitali hiyo kongwe kuanza kutoa huduma hiyo hivi karibuni na kuwapunguzia wakazi wa mkoa huo ambao walilazimika kusafiri hadi Dar es Salaam katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kufuata huduma hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)

Mmoja wa wagonjwa hao, ambaye ni mkazi wa Tanga, Leila Salehe amesema alikuwa akitumia gharama kubwa pindi alipokuwa akipatiwa matibabu.

“Nilipoanza kuumwa sikujua naumwa nini, lakini nilienda Muhimbili, ndipo ikabainika kuwa figo zangu zimefeli.

“Lakini kutokana na kwamba huku Tanga hapakuwa na huduma hii ya kusafisha damu ilibidi nikae kule zaidi ya mwaka mmoja, baada ya huduma huku ilipofunguliwa ikabidi nirudi.

“Dar nilikuwa nakaa mbali… hivyo changamoto ya usafiri ilikuwa inanikumba hasa ukizingatia ilibidi niwe nakodi gari kwa sababu sikuwa na hali nzuri kwa hiyo changamato ya nauli pia ilinisumbua. Lakini hapa Tanga nakaa karibu, tena nakuja peke yangu ninarudi,” amesema.

Madaktari na wagonjwa, wameeleza furaha yao kufuatia uboreshaji huo kubwa ikiwa ni sehemu ya jitihada kubwa za Serikali inayoongozwa na Rais Sami Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya afya.

Akizungumzia upatikanaji wa huduma hiyo mkoani Tanga mmoja wa madaktari bingwa wa Magonjwa ya Dharura, Dk. Juma Ramadhani amesema kutopatikana kwa huduma hiyo mkoani humo kulikuwa changamoto.

“Ilikuwa inatubidi tuwape rufaa wagonjwa wengi kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili

“Pia wagonjwa wengi waliokuwa wanapata huduma nje ya mkoa wa Tanga ilibidi watumie gharama kubwa kwa kukaa mahotelini na nk, lakini ambao ni wakazi wa Tanga sasa wamefanikiwa kurudi mkoani Tanga na kupata huduma hii. Hii imewapunguzia gharama kubwa,” amesema.

Hospitali hiyo ambayo ujenzi wake ulianza mwaka 1896 na kukamilika miaka tisa baadae imepitia maboresho mengi yaliyofanyika katika mara kwa mara.

Zipo huduma muhimu zilizokuwa zikikosekana na kusababisha mateso makali kwa Watanzania waishio Tanga na maeneo ya jirani pindi wanapihitaji huduma hizo.

Moja ya huduma zilizokuwa zinakosekana ni kukosekana kwa huduma za kusafisha damu ambayo sasa imekuwa furaha kwa wakazi wa mkoa huo.

Inaelezwa kuwa awali, wagonjwa walikuwa wanalazimika kufuata huduma hiyo jijini Dar es Salaam na kuweka maisha yao katika hatari zaidi au kuongeza gharama kubwa katika matibabu yao.

error: Content is protected !!