August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mabomu, risasi za 2015 bado hazijatumika

Mwigulu Nchemba

Spread the love

MWIGULU Lameck Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi amesema kuwa kutokana na ugumu wa uchaguzi wa mwaka jana, serikali ililazimika kujiandaa kwa lolote, ikiwemo kununua vifaa vya kijeshi na kiusalama hata hivyo vyote hivyo havikutumika, anaandika Dany Tibason.

Kauli hiyo imetolewa na waziri huyo alipokuwa akizungumza na viongozi wa dini wakiwemo maaskofu na wachungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilitheri Tanzania (KKKT) mkoani Dodoma.

“Kwa hofu ya uchaguzi, serikali ilinunua magari ya washawasha na mabomu na vifaa vingine vya kiusalama huku mataifa ya nje yakiwa yakiwa yanatazamia kuwa lolote linaweza kutokea ikiwa ni pamoja na kutokea kwa vurugu na kupotea kwa amani.

Jambo la uhakikika ni kuwa vifaa hivyo havikutumika hata kidogo. Vipo na havijafanya kazi, ni ukweli usiopingika kuwa amani iliyopo inatokana na maombi ya viongozi wa dini kwa kutumia muda wao mwingi kuliombea Taifa,” alisema Waziri Mwigulu.

Sambamba na hilo, Mwigulu alisema kuwa, serikali inategemea sana taasisi za dini katika kuhamasisha amani nchi hivyo inatopotokea migogoro ndani ya taasisi hizo na kusababisha Jeshi la Polisi kuingilia kati serikali inajikuta katika wakati mgumu.

“Serikali inasimama au kupata amani kutokana na maombi ya viongozi wa dini hivyo si jambo jema ndani ya taasisi za dini kujiingiza katika migogoro hadi kufikia hatua ya Jeshi la Polisi kuwarushia mabomu,” alisisitiza.

Kwa upande wake Dk. Frederick Shoo, Mkuu kanisa la KKKT, alisema kanisa linatimiza majukumu yake ya kuwahudumia watu kimwili na Kiroho.

Hata hivyo, aliitaka serikali kutowaingilia viongozi wa dini pale wanapoishauri au kuikemea.

“Viongozi wa dini, tupo kwa ajili ya kuwajenga watu kimwili na kiroho lakini pale ambapo tunawakosoa hata kama msipopenda inabidi mkubali na si kutushukia au kutuambia kuwa tusichanganye dini na siasa kwani huo ni wajibu wetu,” alisema Dk. Shoo.

error: Content is protected !!