March 7, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mabinti waongoza kupata maambukizi mapya ya VVU

Spread the love

KUNDI la vijana wa kike wenye umri kuanzia miaka 10 hadi 24 limetajwa kuongoza kwa kupata maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (UKIMWI). Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hayo yalibainishwa katika mkutano wa kupitia mipango ya utekelezaji wa afya za ugonjwa wa Ukimwi kwa asasi za kiraia na mitandao ya vijana, na vituo vinavyohudumia watumiaji wa dawa za kulevya ulioandaliwa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) na kufanyika Bagamoyo mkoani Pwani.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mwitikio wa Kitaifa kutoka TACAIDS, Audrey Njeleka amesema asilimia 40 ya maambukizi mapya 81,000 kwa mwaka, yametoka katika kundi la vijana wa kike, na asilimia 80 kwa wanawake kuanzia miaka 15 hadi 24.

Kufuatia changamoto hiyo, Njeleka ametoa wito kwa asasi za kijamii kujiwekea mipango ya kupambana na maambukizi mapya hasa kwenye makundi ya vijana ambayo takwimu zinaonyesha maambukizi yao yako juu.

Aidha, maambukizi mapya ya VVU nchini yamepungua kutoka asilimia 5.1 hadi kufikia 4.7%.

TACAIDS imeitaka jamii kupiga vita maambukizi mapya, na watu wanaoishi na VVU kutumia kikamilifu dawa za kufubaza virusi hivyo (ARVs) bila kukatisha dozi.

error: Content is protected !!