May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mabilioni yamwagwa taasisi za utafiti Tanzania

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa zaidi ya shilingi bilioni tatu kwa taasisi mbalimbali zinazofanya utafiti katika masuala ya kilimo, viwanda, afya na mifungo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pwani … (endelea).

Hayo yamesemwa Jumamosi iliyopita tarehe 3 Julai 2021 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani wakati alipotembelea na kufanya ukaguzi wa namna fedha Sh.400 milioni zilizopelekwa katika Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) zilivyotumika.

Profesa Ndalichako alisema, fedha hizo zilipelekwa katika taasisi hiyo kwa lengo la kuiwezesha kupata vifaa muhimu vinavyotumika katika uthibiti ubora wa chanjo zinazozalishwa nchini pamoja na kufadhili mradi unaolenga kupata mbegu kuu ya chanjo ya magonjwa ya Homa ya Mapafu ya Mbuzi.

“Taasisi hii ni kati ya taasisi zilizopatiwa fedha na wizara kupitia COSTECH ili kuwezesha kufanya utafiti katika eneo lao la mifugo, ninayo furaha kuona fedha walizopata wamezitumia kununulia vifaa muhimu pamoja na kuwapeleka mafunzo wataalamu wao ili kuongeza ujuzi na weledi katika kazi,” alisema Profesa Ndalichako.

Waziri huyo alisema, ufadhali huo umesaidia katika kuongeza tija katika taasisi hiyo, hivyo wizara yake itaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya utafiti ambayo inaendana na malengo ya Maendeleo ya Taifa.

Alisema fedha hiyo siyo fedha nyingi katika utafiti lakini imesaidia kwani ni muhimu kama Taifa kuwa na madawa na chanjo zake yenyewe ambazo zinaaminika.

Aidha ameridhishwa na namna wizara ya mifugo ilivyoweza kusimamia Taasisi yake katika kuhakikisha fedha ambazo wamepata inatumika kama ilivyokusudiwa na kuleta matunda kwa Taifa.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini, Dk. Stella Bitanyi ameishukuru wizara ya elimu kwa ufadhili huo ambao umesaidia Taasisi yake kuongeza ufanisi katika kuzalisha chanjo na kuongeza kiwango cha uzalishaji ambapo mwanzo walikuwa wakizalisha dose milioni 40 lakini baada ya ufadhili imefikia dose milioni 60.

Batinyi aliendelea kueleza ufadhili huo pia umewezesha taasisi hiyo kuzalisha chanjo za kimkakati zinazotumia teknolojia ya cell culture.

Hivyo Wizara ya Elimu imekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha sekta ya mifigo nchini hususan katika kudhibiti magonjwa ya mifugo kupitia chanjo bora zinazoendelea kuzalishwa ambazo hatima yake ni kuwa na mazao mifugo iliyo bora ambayo pia itatoa mazao bora.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk. Amos Nungu amesema kuwa ufadhili unaotolewa kwa ajili ya utafiti unaangalia tafiti ambazo zinaendana na ajenda za maendeleo za Kitaifa. Hivyo utafiti huu pia ni muhimu na unaendana ajenda za maendeleo kupitia Sekta ya Mifugo.

error: Content is protected !!