July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mabilionea walioanza maisha kwa kazi za kawaida

Spread the love

 

INAELEZWA kila mtu anazaliwa tajiri, pia masikini. Utajiri au umasikini wake unategemea na mazingira anayokulia, lakini inategemea zaidi na yeye mwenyewe. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)

Wapo matajiri wengi duniani ambao hawakuzaliwa matajiri. Walitengeneza utajiri wao kwa kupitia maisha ya kawaida ambayo kila mtu ama wengi wa watu wanayaishi.

Kwa mujibu wa jarida la Forbes wapo mabilionea zaidi ya 2,700 duniani, wengi wao walianza kufanya kazi za kawaida kabisa ambazo usingedhani kama wangeweza kuwa mabilionea.

Mabilionea kama Elon Musk, Jeff Bezos, Warren Buffet, Mark Zuckerberg, Steve Jobs, Bill Gates, na Ratan Tata ni mfano wa mabilionea walioanza maisha ya utajiri kwa kufanya kazi za kawaida mtaani au kuajiriwa katika kampuni ndogo na kuishia kuwa matajiri wakubwa duniani.

Jeff Bezos

Huyu ni mmiliki wa kampuni kubwa duniani ya Amazon ambaye kwa sasa ndiye tajiri namba mbili duniani. Lakini Bezos kufika kuwa bilionea namba mbili duniani safari yake imetokea mbali.

Kazi yake ya kwanza alikuwa mpishi, akiandaa vyakula kama baga katika kampuni ya McDonald. Alikuwa na umri wa miaka 16 wakati akifanya kazi hiyo na kulipwa dola 2.69, kwa saa moja.

Mbali na Amazon pia anamiliki The Washington Post aliyoinunua mwaka 2017. Februari 2021, Amazon ilitangaza kuwa Bezos atajiuzulu kama mtendaji mkuu wa kampuni hiyo kuanzia robo ya tatu ya mwaka huu.

Jeff Bezos

Desemba 2013, Bezos alitikisa vichwa vya habari kwa kuanzisha majaribio aliyoyaita “Amazon Prime Air,” ambayo ni utumiaji wa ndege zisizokuwa na rubani kupeleka huduma kwa wateja wake.

Ndege hizo zinaweza kubeba vifurushi vyenye uzito wa mpaka kilo 2.5 na zinaweza kufika umbali wa mpaka maili 10 kutoka ofisi za usambazaji za Amazon.

Elon Musk

Amekulia Amerika Kusini, baadae akahamia Canada akiwa na umri wa miaka 17, na kuanzia kazi ya kawaida kama Mhandisi wa program za kompyuta. Ilikuwa mwaka 1983, alikuwa akiuza michezo ya kompyuta na kulipwa dola 500 kwa mwezi.

Januari 2021, Musk aliripotiwa kumpiku Jeff Bezos kama mtu tajiri zaidi duniani. Inasubiriwa ripoti ya mwaka 2021 kuona matajiri hao wako kwenye nafasi zipi.

Lakini sasa ni tajiri namba tatu duniani akiajiri maelfu ya watu kupitia kampuni zake za Tesla na SpaceX zinazotengeneza roketi, magari ya umeme, umeme wa jua na mabetri akitajwa kuwa na utajiri dola za Marekani 168.2.

Elon Musk

Utajiri wake ulianza kukuwa kwa kasi akiwa na miaka kati ya 25 na 30, akianza kwa kuiuza kampuni yake ya mwanzo ya Zip2 kwenda kuwa sehemu ya Compaq Computers.

Wazazi wake walitengana akiwa na miaka 10, hapo akanza kupenda masuala ya kompyuta.

Alijifunza mwenzewe namna ya kutengeneza programu za kompyuta, akiwa na umri wa miaka 12 tu akauza programu yake ya kwanza, ilikuwa ya mchezo ya kompyuta (game) iliyoitwa Blastar, safari ya utajiri ikaanzia hapo, alikuwa akitengeza na kuuza kwa bei chee kidogokidogo baadae ujuzi wake ukampa fedha na kuwa mmiliki wa kampuni kubwa duniani ya masuala ya teknolojia.

Bill Gates

Bill Gates ni bilionea namba nne duniani, anayefahamika sana na mmiliki wa Kampuni ya Microsoft.

Amekuwa na mchango mkubwa katika Bara la Afrika kupitia taasisi yake na aliyekuwa mkewe ya Bill & Melinda Gates Foundation ambayo imekuwa ikisaidia masuala mbalimbali ya kijamii.

Ameongoza pia kwenye zoezi la kusaidia Chanjo ya Polio kwa watoto barani Afrika.

Lakini hakuanza kama bilionea, alianza kama mfanyakazi wa kawaida kwenye kampuni iliyokuwa ndogo ya TRW, alikuwa mtengeza programu za kompyuta wa kampuni hiyo, lakini sasa ni bilionea namba 4 duniani akiwa na utajiri unaofikia dola bilioni 129.2 kwa mujibu wa Forbes.

Bill Gates alikacha shule akiwa na rafiki yake wa utotoni, Paul Allen na kuamua kuanzisha Microsoft. Hakuwa anaeleweka na familia yake, lakini aliamini katika fikra zake na kwa kuanza kidogokidogo akajikuta anakuwa na kutengeneza utajiri wa kutosha.

Warren Buffet

Warren Buffet, mfanyabiashara na bilionea mkubwa Marekani ambaye kwa mujibu wa mtandao wa Forbes anashika nafasi ya tisa kwa watu wenye utajiri mkubwa duniani.

Alianza kazi ya kusambaza magezeti mtaani, nyumbani na ofisini akifanya kazi hiyo ya kusambaza magazeti ya The Washington Post na kulipwa dola 175 kwa mwezi.

Lakini sasa ni bilionea wa kutupwa akiwa mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Berkshire Hathaway nchini Marekani, ambayo kwa ujumla zimeajiri watu zaidi ya 360,000 na kwa mujibu wa taarifa rasmi za mwaka jana ilikuwa na utajiri wa dola bilioni 42.5.

Werren Buffett

Akiwa na miaka 11 alianza kuwekeza kwenye Kampuni ya Cities Service Preferred akianza kwa kununua hisa tatu tu, ambapo hisa moja iliuzwa kwa dola 38.

Akauza hisa hizo kwa faida kiduchu kwa kuuza hisa moja kwa dola 40, baada ya thamani ya hisa za kampuni hiyo kushuka mpaka dola 27, baadae akajuta baada ya thamani ya hisa kupanda mpaka 200. Anasema majuto hayo ndiyo yaliyomsukuma kufikiria zaidi uwekezaji na kuwa mmiliki wa kampuni kubwa.

Salim Said Bakhresa

Ingawa si bilionea katika orodha ya Forbes, lakini historia yake inamleta kwenye kundi la watu matajiri walioanza kufanya kazi za kawaida mpaka kuwa matajiri wakubwa Afrika. Ni bilionea Afrika akizaliwa visiwani Zanzibar.

Kama ilivyo kwa watoto wengi wa Tanzania na vijana wengi wa nchi hiyo, hupitia kufanya kazi nyingi za kawaida kutokana na uchumi uliopo na mazingira ya nchini.

Bakhresa alianza kuuza mabaki ya mazao ya baharini yanayopatikana kwa wingi hata sasa kwenye fukwe za bahari katika maeneo ya Zanzibar, Dar es Salaam na Mombasa.

Bakhresa hakulala na kuamka tajiri bali alianzia mbali kuusaka utajiri wake.

Alianza kwa kushona viatu, akauza urojo na viazi kabla ya kufungua mgawaha mdogo, lakini leo hii kampuni zake kwenye sekta ya usafirishaji, vinywaji, vyombo vya habari, maji, vyakula, viwanda vya nguo, hoteli na vitu vingine ambazo zimeajiri zaidi ya watu 2,000 na kuingiza mabilioni ya fedha.

Kampuni za Said Salim Bakhresa & Co. (SSB), zinanufaisha zaidi ya watu 6,000 kwa ajira rasmi na zisizo rasmi katika nchi za Afrika Mashariki.

Bidhaa za kampuni zake zinapatikana karibu nchi sita za Afrika Mashariki. Mwaka 2008 alianzisha mpango wa kukabiliana na Malaria baada ya utafiti kuonesha mfanyakazi wake mmoja kati ya watano hukumbwa na malaria kila mwezi.

error: Content is protected !!